Kijamii

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

TV

Nchi

Lifestyle

SIL

MenuKijamiiMaoni
Articles

Nouma anaweza asitoshe kumnyima usingizi Tshabalala

Nouma X Tshabalals Nouma anaweza asitoshe kumnyima usingizi Tshabalala

Tue, 1 Oct 2024 Chanzo: Mwanaspoti

Tusingee sana msimu bado mrefu. Hata hivyo, naanza kupata mawazo kuhusu ule upande wa kushoto wa Mohamed Hussein ‘Tshabalala’ pale Msimbazi. Ameletewa changamoto mpya pale Msimbazi. Jaribio lingine la kumfundisha adabu. Unaweza pia kusema kuchangamsha kikosi.

Katika dirisha kubwa la uhamisho kabla ya msimu kuanza Simba walileta beki wa kushoto, Valentin Nouma kutoka Afrika Magharibi ingawa alikuwa anacheza kwa majirani zetu hapo Congo. Vita SC. Lengo kubwa lilikuwa kuwachangamsha walinzi wa pembeni wazawa ambao kwa muda mrefu wamekuwa wakizihodhi hizi nafasi.

Kwa Tshabalala na Shomari Kapombe muda mrefu sasa tumekuwa tukiwashutumu Simba kwa kuwalinda wachezaji mahiri wa kikosi cha kwanza. Walikuwa hawawaletei upinzani. Hata mchezaji wao wa zamani kama Clatous Chama tuliamini alipaswa kuletewa wachezaji mastaa katika nafasi yake ili kupunguza umuhimu wake klabuni.

Kwa Tshabalala wakati fulani Simba walijaribu kumletea mlinzi wa kushoto wa Ghana, Asante Kwassi kutoka Lipuli ya Iringa. Alianza vyema lakini baadae Tshabalala alirudisha namba yake. Baada ya hapo tumepita kipindi kirefu ambacho Simba wamekuwa wakileta walinzi wa pembeni wa ndani ambao wameonekana kuja kusubiri nafasi zao wakubwa wakiumia. Sio kuwa chaguo la kwanza.

Walikuja kina Israel Mwenda, David Kameta, Gadiel Michael na wengineo. Walikuja kama wasaidizi na sio wenye nafasi zao. Na baada ya muda mrefu kupita ameletwa mlinzi wa kushoto wa kimataifa kutoka taifa la kisoka Afrika Magharibi. Mheshimiwa Nouma. Kuna mambo matatu ya kutafakari kwa haraka haraka.

Kwanza ni namna ambavyo Simba iliachana na bajeti ya walinzi wa pembeni wa bei ghali kwa muda mrefu kwa sababu ya Shomari na Tshabalala. Hawa jamaa wamekuwa katika mwendelezo wa ubora kwa muda mrefu kiasi cha kuwafanya mabosi wa Simba wapambanie zaidi wachezaji wa kigeni wa nafasi nyingine lakini sio za ulinzi wa pembeni.

Nadhani hisia zimeanza kubadilika baada ya watani wao kuanza kufanya vizuri na walinzi wa pembeni wa kimataifa. Kuanzia akina Joyce Lomalisa, Djuma Shaban, Yao Kouassi na sasa Chadrack Boka. Simba wameamua kuwapelekea changamoto kina Tshabalala kwa kuleta wachezaji wa pembeni wa ulinzi wanaotoka huko nje.

Tatizo langu ni moja ni katika hili. Tshabalala ameendelea kuanza na kuupiga mwingi kama kawaida yake. Sioni kama Nouma anaweza kuichukua namba ya Tshabalala kwa kudumu. Tungeweza kubishana kuhusu Tshabalala na Lomalisa. Huyu angeweza kuwa bora kwa mwingine katika jambo fulani. Mashabiki wangeweza kugawanyika.

Kwa sasa Tshabalala angekuwa na wakati mgumu kwa mchezaji kama Boka. Si ajabu ungeweza kuwa mwanzo wa mwisho katika nafasi yake. Lakini kwa Nouma naona Tshabalala ameendelea kuwa yule yule tu. Nouma hatoshi, ana majeraha au Tshabalala ni mzuri zaidi yake? Maana majuzi tu aliitwa katika kikosi cha Burkina Faso timu ya taifa.

Mashabiki wa Simba na mabosi wao wanapomtazama Boka kwa sasa wanajiuliza kwa nini hawakumchukua Boka badala ya Nouma? Boka alikuwa chaguo namba moja pale Vita mbele ya Nouma. Kwanini walikwenda kwa chaguo la pili na sio chaguo la kwanza? Ni mambo yale yale ya Yusuf Kagoma. Nadhani Simba walimuhitaji zaidi Kagoma kuliko Yanga. Hata hivyo Yanga walianza kuhangaika naye mapema kabla ya Simba. Ndio huu mgogoro unaoendelea.

Sasa kuna kila dalili za Tshabalala kuendelea kuitetea nafasi yake bila ya kubadilishana na mtu. Sidhani kama Nouma ametosha katika mafasi ya Tshabalala. Wakati mwingine ni vile tu tunamchukulia poa Tshabalala ni beki bora wa pembeni ukanda huu. Hapana. Ni zaidi ya hapo. Ni miongoni mwa mabeki bora wa pembeni wanaocheza ndani ya bara la Afrika.

Umiliki wa mpira umelala mguuni, pia ana uwiano mzuri wa kulinda na kushambulia. Zaidi ya kila kitu ana mwendelezo wa ubora (consistency).

Tshabalala ni yule yule wa juzi, jana na leo. Shomari kidogo anaonekana kupungua kasi yake katika ule upande wa kulia lakini Tshabalala ameendelea kuwa yule yule tu.

Zaidi ya kila kitu Tshabalala sio msela kama ilivyo kwa wachezaji wengi wazawa. Ana nidhamu na kazi yake ndani na nje ya uwanja. Haishangazi kuona amecheza kiwango cha juu kwa muda mrefu. Ni mchezaji asiyependa starehe na anayejitunza. Anafanya mazoezi kwa nidhamu kubwa kwa muda mwingi.

Mwishoni mwa msimu tutajua kama Nouma amekuja kama walivyokuja akina Gadiel au amekuja kama walivyokuja akina Lomalisa na Boka ambao walikuja kupora nafasi za watu. Vinginevyo mpaka sasa hivi dalili ndogo na haionekani kama Tshabalala anapitia katika tanuri la moto. Uzuri zaidi ni kwamba kwa sasa amekuwa na msaada mkubwa pia kwa Taifa Stars.

Mchezaji ambaye nafasi yake inaonekana kuwa shakani ni Aishi Manula ambaye amepoteza nafasi yake kwa kipa wa kimataifa wa Guinea, Moussa Camara. Sijui atairudishaje tukizingatia pia kwamba Simba walimtoa kafara baada ya kichapo cha mabao 5-1 kutoka kwa mtani wao Yanga msimu uliopita.

Mwingine ambaye kazini kwake kuna kazi ni Mzamiru Yassin. Kwa muda mrefu amekuwa akipendwa na kila kocha anayepita Msimbazi lakini kwa sasa ana mtihani mkubwa kwa mafundi, Deborah Hernandes na Yusuf Kagoma. Tofauti na yeye, wao wana ufundi mwingi mguuni nje ya kujituma zaidi uwanjani.

Pamoja na yote haya lakini ni wazi kwamba Simba wameanza kuwa na kikosi kipana. Wameanza kuwa na benchi ambalo unaweza kulitumainia kama mambo yakienda kombo ndani ya uwanja. Watani wao Yanga swalishatengeneza timu ya namna hii kwa muda mrefu sasa. Kila mchezaji ni chuma. Ndani na nje ya uwanja

Columnist: Mwanaspoti
Related Articles: