Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

TV

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Idadi vifo ajali ya Geita vyafika nane, majeruhi 49

Ajali Get Idadi vifo ajali ya Geita vyafika nane, majeruhi 49

Wed, 8 Mar 2023 Chanzo: mwanachidigital

Idadi ya waliofariki katika ajali ya Basi la Sheraton lililokuwa likifanya safari zake kutoka jijini Mwanza kwenda Ushirombo mkoani Geita iliyotokea jana Machi 7, 2023 katika eneo la Ibandakona wilayani Geita, imeongezeka na kufikia watu wanane baada ya mmoja kupoteza maisha wakati akipatiwa matibabu katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Geita.

Mkuu wa mkoa wa Geita Martine Shigella Akizungumza na mtoto ambae ni mmoja wa majeruhi aliyepata ajali katika basi la Sheraton linalofanya Safari zake kutoka Mwanza kwenda Ushirombo.mtoto huyo ni miongoni mwa watoto watatu ambao hawajafahamika walikua na nani kwenye gari hilo.

Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya Rufaa Geita, Dk Mfaume Salum akizungumza asubuhi ya leo amesema majeruhi mmoja kati ya 50 waliokuwa wamefikishwa hospitalini hapo alifariki dunia wakati madaktari wakijitahidi kuokoa maisha yake.

Dk Salum amesema hadi sasa majeruhi walioko hospitalini hapo ni 49 ambapo wanaume ni 25 na wanawake 24 na waliofariki papo hapo kwenye ajali ni watu saba kati yao wanawake ni wanne na wanaume watatu pamoja na majeruhi mmoja aliyefariki wakati akipatiwa matibabu.

Amesema majeruhi wanne ambao hali zao hazikuwa nzuri wamepewa rufaa kupelekwa Hospitali ya Kanda Bugando kwa matibabu zaidi.

Kaimu Kamanda wa Polisi Mkoa wa Geita, Berthaneema Mlay amesema chanzo cha ajali ni tairi ya mbele ya gari kupasuka na kusababisha gari kutumbukia kwenye korongo na kwamba uchunguzi wa awali unaonyesha dereva alikuwa kwenye mwendo wa kasi.

Akizungumza baada ya kutembelea majeruhi waliolazwa hospitalini hapo, Mkuu wa Mkoa wa Geita Martine Shigella amelitaka Jeshi la Polisi kuchunguza na kukagua vyombo vya usafiri kama vinafaa kuendelea na safari sanjari na kuwakagua na kuwachukulia hatua madereva wanaoendesha kwa mwendo wa kasi barabarani ili sheria iweze kuchukua mkondo wake.

Hii ni tukio la pili la ajali barabarani kutokea ndani ya wiki hii na kusababisha vifo ambapo Machi 6, 2023 hii watu tisa walipoteza maisha na wengine 30 kujeruhiwa baada ya basi linalofanya safari kutoka Kigoma kwenda Mpanda kuacha njia na kupinduka

Chanzo: mwanachidigital
Related Articles: