Mapigano kati ya jeshi la Sudan na kikosi chenye nguvu cha kijeshi yamesababisha watu zaidi ya milioni 1.3 kukoseshwa makazi. Shirika la uhamiaji la Umoja wa Mataifa lilisema siku ya Jumatano.
Shirika la Kimataifa la Uhamiaji limesema mapigano hayo yamewalazimisha watu zaidi ya milioni moja kuyahama makazi yao na kwenda katika maeneo salama ndani ya Sudan. Wengine wapatao 320,000 wamekimbilia nchi jirani za Misri, Sudan Kusini, Chad, Ethiopia, Jamhuri ya Afrika ya Kati na Libya.
Mapigano hayo yalizuka tarehe 15 Aprili, baada ya miezi kadhaa ya mivutano mikali kati ya jeshi linaloongozwa na Jenerali Abdel-Fattah Burhan, na Vikosi vya Rapid Support Forces vinavyoongozwa na Jenerali Mohamed Hamdan Dagalo.
Mzozo huo umevuruga matumaini ya Wasudan ya kurejesha kipind tete mpito kuelekea demokrasia, ambacho kiliingiliwa kati na mapinduzi ya kijeshi yaliyoongozwa na majenerali hao wawili mwezi Oktoba 2021.
Mgogoro huo umesababisha vifo vya raia takriban 863, wakiwemo watoto wasiopungua 190, na kujeruhi watu wengine zaidi ya 3,530, kulingana na idadi iliyotolewa hivi karibuni na Muungano wa Madaktari wa Sudan - ambao unafuatilia sana idadi ya vifo vya raia. Pia mgogoro huo umeifanya nchi hiyo ya Afrika Mashariki kukaribia kuvunjika, huku maeneo ya mijini katika mji mkuu wa Khartoum, na mji jirani wa Omdurman kugeuka kuwa uwanja wa vita.
Missri ni mwenyeji wa idadi kubwa zaidi ya watu waliokimbia vita, ikiwa imechukua watu wasiopungua 132,360, ikifuatiwa na Chad yenye watu 80,000 na Sudan Kusini yenye watu zaidi ya 69,000, shirika hilo la Uhamiaji liliongeza.
Mapigano ya hapa na pale bado yaliendelea siku ya Jumatano katika maeneo kadhaa, licha ya usitishaji mapigano uliofikiwa wiki hii. Wakaazi waliripoti kusikia milio ya risasi na milipuko katikati mwa Khartoum pamoja na maeneo ya karibu na vituo vya kijeshi huko Omdurman.
Usitishaji wa mapigano ya wiki nzima, ambayo yalisimamiwa na Marekani na Saudi Arabia, ulianza kutekelezwa siku ya Jumatatu usiku. Ilikuwa ni juhudi za hivi karibuni za kimataifa za kuweka msukumo katika upelekaji wa misaada ya kibinadamu katika nchi hiyo yenye mgogoro.
Katika taarifa ya pamoja ya Marekani na Saudi Arabia jana Jumanne ilionya kwamba jeshi la Sudan pamoja na Vikosi vya Support Forces lazima zifuate kanuni za usitishaji huo wa muda mfupi wa mapigano .