Umoja wa Mataifa unasema vita vya Sudan ambavyo vimedumu kwa mwezi sasa vimesababisha takriban watu milioni moja kuyahama makazi yao. Wengi wao wakisalia ndani ya nchi hiyo.
Licha ya makubaliano ya kusitisha mapigano yaliyofikiwa kati ya jeshi na kikosi maalum cha wanamgambo cha Rapid Support Forces RSF, pande hizo mbili zimeendelea kupigana hata katika maeneo ya makazi katika mji mkuu Khartoum.
Mapigano hayo yamesababisha mzozo mkubwa wa kibinadamu Sudan. Maafisa wa Sudan wamekuwa wakikutana na wajumbe wa mashirika ya Umoja wa Mataifa kujadili namna ya kuudhibiti mzozo huo na jinsi ya kufikisha misaada ya kibinadamu kwa waathiriwa wa vita hivyo.
Mnamo tarehe 15 Aprili 2023,mzozo kati ya Jeshi linaloongozwa na Jenerali Abdel Fattah al-Burhan na kikosi maalumu cha wanamgambo wa kikosi maalum cha RSF kinachoongozwa na Mohamed Hamdan Daglo ulitibuka kuwa vita,ukianzia katika kitovu cha nchi hiyo,jijini Khartoum.
Mji huo wa takriban watu milioni tano uligeuka kuwa uwanja wa mapambano,milio ya risasi ikirindima na mabomu yakifyatuliwa kila kona. Hospitali,benki,maduka na maghala ya chakula yaliporwa na kuharibiwa.
Wafanyakazi wa kutoa misaada walishambuliwa na wengine hata kuuuawa.Nchi za kigeni zilikimbia kuwaondoa raia wao. Mzozo wa Sudan umesababisha vifo vya takriban watu mia saba,maelfu wamejeruhiwa na takriban watu milioni moja kuachwa bila ya makazi ndani ya nchi huku wengine wakikimbilia nchi jirani zikiwemo Sudan Kusini,Ethiopia,Chad na Misri.
Upatikanaji wa bidhaa za kimsingi ni tabu na bei za vyakula na mafuta zimeongezeka maradufu. Makubaliano ya kusitisha vita hivyo yamefikiwa mara chungu nzima lakini yamekiukwa hata kabla wino ulioandikia makubaliano hayo kukauka na hivyo kudidimiza matumaini ya kupatikana suluhu la mzozo huo hivi karibuni.
Umoja wa Mataifa,Umoja wa Afrika,Marekani,nchi za kiarabu zikiongozwa na Saudi Arabia zote zimejaribu kuwa mpatanishi katika mzozo huu wa Sudan lakini bado pande zote mbili zikikataa kulegeza kamba.
Na kwa nchi ambayo tayari ilikuwa katika msukosuko wa kisiasa tangu kupinduliwa madarakani kwa Rais Omar Bashir na jeshi na maeneo kama Darfur yakikumbwa na mzozo wa kibinadamu kwa miongo kadhaa,mashaka ni mengi kuliko matumaini Sudan.