Umoja wa Mataifa umetoa wito wa ufadhili wa dola bilioni tatu kwa ajili ya Sudan kuweza kutoa misaada ya kiutu katika taifa hilo linalikumbwa na mzozo na mataifa jirani ambayo yanahifadhi wakimbizi kutoka Sudan.
Maelfu ya watu wameachwa bila ya makazi tangu mzozo kuzuka kati ya Jeshi na kikosi maalum cha wanamgambo cha Rapid Support Forces mwezi uliopita na hivyo kusababisha janga la kibinadamu nchini humo.
Mzozo huo unaendelea bila ya kusita licha ya makubaliano kadhaa kufikiwa ya kusitisha mapigano na kuruhusu misaada ya kibinadamu kufikia raia walioathirika. Inaaminika takriban watu milioni moja wamelazimika kuyahama makazi yao.
Hospitali zimeshambuliwa na kuharibiwa,huduma za umeme na maji zimekatwa huku kukiripotiwa ukiukaji mkubwa wa haki za binadamu ikiwmo kuuawa kiholela na wanawake kubakwa.
Hata kabla ya mzozo huu,Sudan ilikuwa inakabiliwa na mahitaji makubwa ya kibinadamu kufuatia mizozo ya kipindi cha nyuma na imekuwa ikiwahifadhi maelfu ya wakimbizi kutoka nchi jirani za Ethiopia na Sudan Kusini.