Mji mkuu wa Sudan, Khartoum, unakabiliwa na mapigano makali baina ya vikosi hasimu.
Ndege za kijeshi aina yajeshi za Sudan zinaendelea na mashambulizi ya anga na kwenye miji iliyo karibu ya Bahrin na Omdurman, licha ya mazungumzo ya kusitisha mapigano yanayofanyika nchini Saudi Arabia.
Mapigano ya ardhini pia yanaendelea kati ya jeshi la wanajeshi wa kikosi cha dharura - Rapid Support Forces (RSF) katika maeneo mawili katikati miji ya Bahri - Shambat na Halfiya.
Mapigano katika eneo la Shambat yapo karibu na ngome kubwa ya jeshi, huku mapambano ya Halfiya yanaonekana kulenga udhibiti wa daraja muhimu, ambalo kwa sasa liko mikononi mwa RSF.
Lakini watu wengi bado wana matumaini kwamba mazungumzo yanayoendelea nchini Saudi Arabia -ambayo ni ya kwanza baina ya pande hizo zinazohasimiana – yatawezesha kusitishwa kwa mapigano, ingawa mwanadiploamasia ambaye hakutajwa jina ameliambia Shirika la habari la AFP kwamba ‘’hakuna mafanikio makubwa’’ yaliyofikiwa hadi sasa.
Wakati huohuo, jeshi limewakamata wanaharakati wawili wanaounga mkono katika mji wa Bahri, wakiwashutumu kwa kuunga mkono RSF.
Wenzao wamedai kuachiliwa kwao mara moja, wakisema madai dhidi yao ni ya uongo.
Kamati za kujilinda mjini humo – zilizoundwa kwa ajili ya kukampeni kuwepo kwa demokrasia nchini Sudan -zimekuwa na nafasi muhimu katika kutoa msaada wa kibinadamu kwa wakazi tangu vita vilipoibuka tarehe 15 Aprili.
Mkuu wa majeshi wa Sudan Abdel Fattah al-Burhan na kamanda wa RSF Mohamed Hamdan Daglo kwa pamoja walifanya mapinduzi mwaka 2021, lakini sasa wanapiagania madaraka, jambo linaloondoa matumaini ya kuwepo kwa kipindi cha mpito kuelekea utawala wa kiraia nchini Sudan.