Shirika la Marekani la Maendeleo ya Kimataifa (USAID) linatuma timu ya wataalam wa kukabiliana na majanga ili kuratibu mwitikio wa kibinadamu nchini Sudan huku kukiwa na mapigano kati ya makundi hasimu ya jeshi.
Samantha Power, mkuu wa shirika hilo, alisema Jumapili kwamba wataalamu hao watafanya kazi na washirika wa kimataifa kutambua mahitaji ya kipaumbele na kutoa msaada kwa wale wanaohitaji.
Timu hiyo itakuwa ikifanya kazi kutoka Kenya katika awamu ya awali ya shughuli zake, shirika hilo lilisema.
Bi Power alisisitiza wito wa jumuiya ya kimataifa wa kusitisha mapigano na kukomesha umwagaji damu. "Marekani inavitaka Vikosi vya Wanajeshi vya Sudan na Vikosi vya Msaada wa Haraka kutii usitishaji vita wa siku tatu wa Eid al-Fitr ambao wamekubali, kukomesha umwagaji damu huu usiojali, kuwezesha upatikanaji wa huduma za kibinadamu, kuzingatia sheria za kimataifa za kibinadamu," alisema.
Zaidi ya watu 400 wameuawa katika mapigano hayo na maelfu kujeruhiwa katika ghasia hizo ambazo sasa zimeingia wiki yake ya pili.