Wakati nchi za Ulaya na Marekani zikiendelea na juhudi za kuwaondoa raia wale kutoka Sudan kutokana mapigano makali yanayoendelea, baadhi ya nchi za Afrika ambazo raia wake wapo nchini humo wanaonekana kukata tamaa.
Mwanafunzi kutoka nchini Nigeria aliyeko katika mji mkuu Khartoum, ambaye hakutaka kutaja jina lake, anasema anahisi serikali ya nchi yake imemtelekeza. Anasema ni vigumu kwa jinsi hali ilivyo kwa sasa kupata njia ya kuondoka.
Tanzania wiki jana ilisema ina mpango wa kuwarejesha raia wake walioko nchini Sudan lakini haijatoa maelezo ya hatua zilizopigwa kufanikisha hilo hadi sasa.
"Serikali imeendelea kufanya mawasilano ya mara kwa mara na ubalozi wetu uliopo mjini Khartoum, ili kujua hali inavyoendelea. Tunao watanzania takriban 210 nchini Sudan ambapo 171 kati ya hao ni wanafunzi, na wengine na maafisa wa ubalozi na raia wengine. Hadi sasa hakuna mtanzania aliyeripotiwa kuathiriwa na mapigano hayo. Namshukuru balozi wetu kwa kuhakikisha usalama wa raia wetu nchini humo,” alisema Waziri wa Mambo ya Nje wa Tanzania Stergomena Tax Jumatano wiki iliyopita.
Kenya kwa upande wake imeanzisha operesheni ya kuwahamisha raia wake kutoka Sudan kutokana na mzozo unaoendelea kati ya Jeshi la Sudan na Kikosi cha Msaada wa Haraka (RSF), ambao sasa umeingia wiki yake ya pili.
Kenya sasa inaungana na nchi nyingine zikiwemo Marekani, Uingereza, Ufaransa, Ujerumani na Canada ambazo tayari zimewahamisha baadhi ya raia wake.
Waziri wa Mashauri ya Kigeni Alfred Mutua ametangaza kuwa nchi jirani zikiwemo Sudan Kusini, Ethiopia, Misri na Saudi Arabia zimetoa ruhusa kwa ndege za Kenya kuruka juu ya anga zao ili kuwahamisha Wakenya waliokwama nchini Sudan.
Alishukuru serikali za Sudan Kusini na Ethiopia kwa kukubali ombi la Kenya la kuwaruhusu raia wa Kenya kuvuka mipaka yao na kufikia maeneo salama.
Mutua alifichua kuwa Wizara ya Masuala ya Kigeni ina programu tatu za kuwahamisha watu.
Tayari wamewavukisha wanafunzi 29 wa Kenya hadi Ethiopia, ambapo watasafiri kwa ndege hadi Gondor na kisha Addis Ababa kabla ya kuelekea Nairobi.
Zaidi ya hayo, ndege ya Kenya Airforce imetumwa kulihamisha kundi la wanafunzi 18 wanaosafiri kwa barabara kwa sasa hadi mpaka wa Sudan Kusini.
Kulingana na Mutua, kundi kubwa la Wakenya litahamishwa kupitia ndege mbili kutoka Port Sudan hadi Jeddah, na kisha kusafiri hadi Nairobi kutumia shirika la Kenya Airways.
Anakadiria kuwa "Wakenya 300-400, ikiwa sio zaidi," watahamishwa kupitia njia hii.
Hapa kuna muhtasari mfupi wa kile kilichotokea hadi sasa katika oparesheni ya nchi mbali mbali kuwaokoa raia wake
Marekani, Canada na Uingereza zilitangaza Jumapili kuwa zimewasafirisha wanadiplomasia wake kutoka Sudan.
Rais wa Ufaransa Emmanuel Macron alithibitisha kwamba uhamishaji ulifanyika Jumapili na Jumatatu, na kuwapata raia 388 na wanadiplomasia kutoka Sudan.
Raia wachache wa Uholanzi pia waliondoka Khartoum kwa ndege za Ufaransa. Jeshi la Ujerumani limesema ndege ya kwanza kati ya tatu iliondoka Sudan, kuelekea Jordan, ikiwa na watu 101.
Italia na Uhispania zimewahamisha raia - misheni ya Uhispania ilijumuisha raia kutoka Argentina, Colombia, Ireland, Ureno, Poland, Mexico, Venezuela na Sudan. Uturuki- mhusika mkuu nchini Sudan - ilikusanya watu 640 katika mabasi 13 ili kuwahamisha kwa barabara - wengine 500 walikusanyika katika sehemu ya uokoaji.Ujumbe huo ulijumuisha raia kutoka Azerbaijan, Japan, China, Mexico na Yemen.
Zaidi ya raia 1,000 wa Umoja wa Ulaya wamehamishwa, mkuu wa sera za kigeni wa umoja huo Josep Borrell alisema Jumatatu, hasa akiishukuru Ufaransa kwa operesheni hiyo.
Zaidi ya watu 150, wengi wao wakiwa raia wa nchi za Ghuba, pamoja na Misri, Pakistanna Kanada wamehamishwa kwa njia ya bahari hadi kwenye bandari ya Saudi Arabia ya Jeddah.