Mapigano makali kati ya pande zinazozozana yameendelea katika mji mkuu wa Sudan, Khartoum na miji mingine kabla ya mazungumzo ya kusitisha mapigano siku ya Jumapili.
Wakaazi wanasema jeshi la Sudan limeshambulia maeneo ya raia, huku Kikosi cha Rapid Support Forces (RSF) kikichukua mali za raia.
Mapigano yaliripotiwa mjini Khartoum, nchi jirani za Omdurman na Geneina katika eneo la Darfur.
Vita kati ya jeshi la nchi hiyo na RSF vilianza karibu mwezi mmoja uliopita.
Mkazi mmoja Hani Ahmed, 28, alisema hali ilikuwa mbaya zaidi asubuhi ikilinganishwa na siku mbili zilizopita.
"Ungeweza kusikia vizuri mizinga na RSF walikuwa wakishika doria mitaani kuliko kawaida," aliongeza.
"Tunaona tu jeshi angani, lakini katika suala la mawasiliano ya ana kwa ana, tunaona tu kikosi cha RSF. Ndio walio chini," Bw Ahmed alisema.
Mamia wameuawa na karibu 200,000 wametoroka makazi yao na kuelekea majimbo jirani huku watu 700,000 wameondoka makazi yao ndani ya nchi.
Uporaji ulioenea, pamoja na kuondoka kwa mashirika ya misaada ya kimataifa, umesababisha uhaba mkubwa wa chakula na dawa.
Watu waliotoroka makazi yao wanaoishi katika kambi kubwa kaskazini mwa Darfur wamepunguza mlo mmoja kwa siku.
Shirika la misaada la kimatibabu la Medecins Sans Frontieres (MSF) lilionya kuwa hali za watoto zinaweza kuzorota.
Pande zinazozozana zilitia saini "tamko la kujitolea" siku ya Alhamisi, baada ya wiki moja ya mazungumzo yaliyopatanishwa na wenyeji Saudi Arabia na Marekani.
Mazungumzo ya kusitisha mapigano kati ya wawakilishi wa pande zinazozozana yataanza tena mjini Jeddah siku ya Jumapili.