Mashambulizi ya anga yameathiri mji mkuu wa Sudan, Khartoum, licha ya mapatano yaliyolenga kuwaruhusu raia kukimbia hadi maeneo salama.
Jeshi lilisema lilikuwa linashambulia jiji hilo ili kuwaondoa wapinzani wake wa kijeshi, Kikosi cha (RSF).
Mapigano hayo yalizidi kupamba moto huku pande zinazozozana zikisema kwamba zitaongeza muda wa makubaliano hayo kwa siku tatu nyingine.
Zaidi ya vifo 500 vimeripotiwa huku idadi halisi ya majeruhi ikiaminika kuwa kubwa zaidi.Mamilioni ya watu bado wamenaswa mjini Khartoum.
Kamanda wa jeshi Jenerali Abdel Fattah al-Burhan na mkuu wa RSF Jenerali Mohamed Hamdan Dagalo, anayejulikana zaidi kama Hemedti, wanawania mamlaka - na hawakubaliani hasa kuhusu mipango ya kujumuisha RSF katika jeshi.
Majenerali hao walikubali kusitisha mapigano kwa sababu za kibinadamu baada ya juhudi kubwa za kidiplomasia za nchi jirani, Marekani, Uingereza na Umoja wa Mataifa.Makubalino hayo hata hivyo hayajapelekea kusistishwa kwa vita .
Hata hivyo, bado haijafahamika ni nini watafanya katika hatua inayofuata ya makubaliano yaliyofikiwa na upatanishi wa Marekani na Saudi, kulingana na jeshi.
Nchi hiyo sasa inapigana vita vya wenyewe kwa wenyewe, anasema mfanyabiashara na Mhisani wa Sudan Mo Ibrahim, na mzozo wake haufai kuruhusiwa kuenea katika nchi jirani .
"Hatutaki Syria nyingine," aliambia BBC, na kuongeza kuwa ilikuwa vigumu kwa kila upande kushinda moja kwa moja.