Marekani na Saudi Arabia zimeafiki kurefushwa kwa makubaliano ya muda wa kusitisha mapigano kati ya pande zinazozohasimiana nchini Sudan kwa siku nyingine tano.
Serikali za Washington na Riyadh zilitangaza makubaliano ya hivi punde zaidi, na vile vile kuafikiana kuhusu makubaliano ya wiki moja iliyopita.
Katika taarifa yao ya pamoja, wamekiri kwamba usitishaji mapigano haujazingatiwa kikamilifu, lakini wakasema umeruhusu kufikishwa kwa misaada kwa watu milioni mbili nchini Sudan.
Shirika la Mpango wa Chakula Duniani lilisema kuwa hali ya utulivu katika mapigano iliiruhusu kutuma vifaa kwa wakazi waliokwama katika mji mkuu, Khartoum, kwa mara ya kwanza tangu mapigano yalipozuka wiki sita zilizopita.
Jeshi la Sudan na wapinzani wake kutoka kikosi cha dharura wameshutumiana kwa ukiukaji wa mara kwa mara wa makubaliano ya usitishaji mapigano, hasa katika eneo la Darfur.