Mapigano yalisikika kusini mwa Khartoum siku ya Jumapili wakati wajumbe kutoka pande zinazozozana nchini Sudan walikuwa nchini Saudi Arabia kwa ajili ya mazungumzo ambayo wapatanishi wa kimataifa wanatumai kuwa yatamaliza mzozo uliodumu kwa wiki tatu ambao umeua mamia na kusababisha watu wengi kuhama makazi yao.
Mpango huo wa Marekani na Saudia Arabia ni jaribio la kwanza kubwa la kusitisha mapigano kati ya jeshi na kikosi cha RSF ambayo yamegeuza sehemu za mji mkuu wa Sudan Khartoum kuwa uwanja wa vita na kurudisha nyuma mpango unaoungwa mkono kimataifa wa kuanzisha utawala wa kiraia kufuatia miaka kadhaa ya ghasia na machafuko.
Mapigano tangu katikati ya mwezi wa Aprili yamesababisha vifo vya mamia ya watu na kujeruhi maelfu wengine, kuvuruga usambazaji wa misaada na kupelekea wakimbizi 100,000 kukimbilia nje ya nchi.