Shinikizo la kidiplomasia linaongezwa ili kusitishwa mapigano nchini Sudan ambayo yamesababisha vifo vya zaidi ya watu 300 katika wiki moja.
Jeshi la Sudan limekuwa likipambana na wanamgambo wanaoitwa Rapid Support Forces (RSF).
Umoja wa Mataifa, Marekani na mataifa mengine yamekuwa yakishinikiza kusitishwa kwa vita kwa muda wa siku tatu kuadhimisha sikukuu ya Waislamu ya Eid al-Fitr.
RSF inasema imekubali kusitisha mapigano ya saa 72 kwa misingi ya kibinadamu.
Hakukuwa na maoni ya kutoka kwenye jeshi la kawaida. Usitishaji vita utakuwepo kuanzia saa 06:00 (04:00 GMT) siku ya Ijumaa ili iendane na sikukuu, RSF ilisema.
Majaribio mawili ya awali ya kusitisha mapigano yalishindwa kutekelezwa.
Mkuu wa jeshi, Jenerali Abdel Fattah al-Burhan, awali alipuuza uwezekano wa mazungumzo na RSF.
Matumaini ya hivi karibuni ya kupatikana kwa mapatano ya muda yalikuja baada ya Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa António Guterres kutoa wito wa kusitishwa kwa mapigano ili kuruhusu raia kupata usalama.
Usitishaji vita kwa ajili ya Eid "lazima iwe hatua ya kwanza katika kutoa ahueni ya mapigano na kuandaa njia ya usitishaji mapigano wa kudumu", Bw Guterres alisema.
"Usitishaji huu wa mapigano ni muhimu kabisa kwa sasa," aliongeza.
Eid ni sikukuu ya Waislamu inayoashiria mwisho wa mfungo wa Ramadhani.
Umoja wa Mataifa umeonya kuwa kati ya watu 10,000 hadi 20,000 - wengi wao wakiwa wanawake na watoto wamekimbia Sudan kutokana na mapigano makali huko ili kutafuta usalama katika nchi jirani ya Chad.