Safari ya mwisho ya msanii wa Ndogo Jaraah aliyeaga dunia katika ajali, imewaacha jamaa na marafiki wakiwa na simanzi nyingine baada ya gari lililokuwa limebeba maiti yake kumgonga na kumuua dereva bodaboda nchini Kenya.
Keshy Aluoch Owuor, ambaye alikuwa rafiki wa karibu wa marehemu Ohangla amezungumzia tukio hilo na kusema kuwa ajali hiyo ilimuua dereva bodaboda katika eneo la Lela kwenye barabara Kuu ya Kisumu kuelekea Busia nchini humo.
Keshy alisema kuwa wakati ajali hiyo inatokea, tayari walikuwa wameshatoka kuchukua mwili wa marehemu kutoka chumba cha kuhifadhia maiti wakiupeleka nyumbani.
“Ni jambo la kuhuzunisha kwa sababu Ndogo aliaga dunia na wanabendi wake watatu katika ajali ya gari iliyotokea katika Barabara Kuu ya Nairobi kuelekea Kisumu, lakini gari lililokuwa limebeba mwili wake nalo likahusika katika ajali ya barabarani ambayo iligharimu maisha ya bodaboda huyo,” alisema Keshy.
Awali iliarifiwa kuwa familia na marafiki wa msanii huyo wa Ohangla walibaki kuomboleza kuafuatia kifo chake cha ghalfa kufuatia ajali ya barabarani kwenye barabara kuu ya Nairobi kuelekea Kisumu.
Ndogo alipata ajali na wenzake akiwa safarani kuelekea Kisumu baada ya kutumbuiza jijini Nairobi.