Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Wanavyomzungumzia Lowassa mitandaoni

Lowassa Deaddd).jpeg Waziri Mkuu Mstaafu wa Tanzania, Edward Lowassa

Sat, 10 Feb 2024 Chanzo: Mwananchi

Majonzi na simanzi vimetawala kwenye mitandao ya kijamii kufuatia kifo cha mwanasiasa mkongwe na Waziri Mkuu mstaafu, Edward Lowassa kilichotokea leo Februari 10, 2024 jijini Dar es Salaam.

Mwanasiasa huyu amefariki dunia akipatiwa matibabu katika Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete (JKCI), alikokuwa akitibiwa maradhi matatu tofauti ambayo ni mapafu, shinikizo la damu na utumbo kujikunja.

Makamu wa Rais, Dk Philip Mpango ndiye aliyetangaza kifo hicho na kueleza kuwa Rais Samia Suluhu Hassan ametoa siku tano za maombolezo.

Wanasiasa na viongozi mbalimbali wameonyesha kuguswa na kifo hicho, na kueleza namna ambavyo mwanasiasa huyo aligusa maisha yao na mchango wake kwa Taifa.

Kupitia ukurasa wake wa Instagram, Katibu wa Rais, Waziri Salum amemtaja Lowassa kama kiongozi aliyekuwa na uwezo wa kutambua na kuibua vipawa vya uongozi kwa vijana.

“Mzee mwema mwenye uwezo wa kutambua, kuibua, kuvisimamia, kuviongoza na kuvipa nguvu vipawa vya uongozi kwa vijana wengi. Nakumbuka mwaka 2014 kwenye Bunge Maalumu la Katiba, aliniita siku moja akaniambia ‘napenda vijana wenye akili nyingi, tafuta jimbo ugombee, nitakusaidia na utashinda, hatuwezi kuacha vijana kama wewe mkapotelee kusikojulikana’. Asante kwa kuniamini na kuona kitu ndani yangu,” amesema Salum.

Aliyekuwa Katibu Mkuu wa CCM, Daniel Chongolo ameandika: “Nimepokea kwa masikitiko taarifa ya kifo cha Waziri Mkuu mstaafu, Edward Lowassa, natoa pole kwa familia na Watanzania wote kwa kuondokewa na kiongozi wetu aliyewahi kuhudumu nafasi mbalimbali katika siasa na Serikali ya JMT. Apumzike kwa amani.”

Salamu kama hizo zimetolewa pia na Mbunge wa Segerea, Bonna Kamoli kupitia ujumbe alioandika kwenye ukurasa wake wa Instagram ukisomeka, “Kama Taifa tumempoteza kiongozi shupavu muwajibikaji na mwanasiasa nguli, Mungu awajalie ndugu jamaa na marafiki nguvu faraja hasa katika kipindi hiki cha kuondokewa na mpendwa wetu.”

Boniface Jacob, meya wa zamani wa Ubungo na mjumbe wa kamati kuu ya Chadema, chama ambacho Lowassa aliwahi kujiunga na kupeperusha bendera akiwania nafasi ya urais katika uchaguzi wa mwaka 2015, amemtaja mwanasiasa huyo kama jabali la siasa.

“Jabali la siasa limeondoka. Mtu muungwana ametangulia. Rafiki amelala usingizi wa milele. Kiongozi wa watu ametamatika. Mzee Lowassa ilikuwa ni shule ya siasa na uongozi iliyokuwa inatembea, tuliobahatika kuwa naye karibu tumeachiwa utajiri wa maarifa,” unasomeka ujumbe wa Jacob.

Mkurugenzi Mtendaji wa EFM, Francis Ciza, maarufu Majizzo naye ameandika, “Kichwa chini, Edward Ngoyai Lowassa hatupo naye. Tutamkumbuka kama kiongozi aliyeacha alama ya mapambano kwenye uwajibikaji, medani za siasa na uongozi”.

“Nenda Edo pumzika kwa amani. Tutamkumbuka kwa misimamo katika mambo aliyokuwa akiyaamini, buriani Leigwanani, buriani mtu mwenye roho ya aina yake,” ameandika Addo Novemba.

Chanzo: Mwananchi
Related Articles: