Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Kisa cha Diana Chilolo kufuta namba ya Lowassa

Diana Chilolo Lowassa Kisa cha Diana Chilolo kufuta namba ya Lowassa

Tue, 13 Feb 2024 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Aliyekuwa mbunge wa viti maalumu Mkoa wa Singida, mwaka 2000 hadi 2015, Diana Chilolo ameeleza namna alivyofuta namba ya simu ya Waziri Mkuu mstaafu Edward Lowassa, baada ya kutangaza kuondoka CCM na kujiunga na Chadema.

Chilolo ametoa kauli hiyo jana Jumatatu, Februari 12, 2024 alipozungumza na Mwananchi Digital akiwa mkoani Singida.

Amesema Lowassa alikuwa rafiki yake na hata mafanikio aliyopata kisiasa alipokuwa bungeni yalikuwa na mchango mkubwa wa mwanasiasa huyo mkongwe nchini.

Chilolo amesema licha ya urafiki wao, alilazimika kufuita namba ya simu ya Lowassa alipotangaza kujiunga na Chadema, kwa kuwa alishindwa kuhamia upinzani kutokana na imani yake kubwa kwa CCM.

“Lowassa alipotangaza nia kugombea urais kupitia CCM nilikuwa naye jukwaani na nilimuunga mkono kwa asilimia 100 kwa sababu alikuwa rafiki yangu, hivyo nilikuwa naye kwenye kila jambo alilofanya.Lakini apoamua kuhamia upinzani kwa kweli tulitofautiana, nililazimika kufuta hadi namba yake ya simu,” amesema Chilolo.

“Urafiki baina yangu na Lowassa ulikufa baada ya kuhamia upinzani maana nilijitahidi kumshauri aache kwenda upinzani kwa sababu tumefanya mengi ndani ya chama, lakini alisema nia yake ni kuwa rais, hivyo hawezi kuendelea kuwa mwana-CCM,” amesema.

Amesema bungeni walikuwa wakikaa viti jirani, hivyo alikuwa akimsaidia kwa mambo mengi yanayohusu siasa za kitaifa na za kimataifa, ndiyo maana alikuwa na uwezo wa kuuliza maswali mengi bungeni bila kukosea.

“Alipoona nimesimama nataka kuuliza swali alikuwa ananiuliza unataka kusema nini Diana? nilikuwa namweleza nilichokuwa nataka kukisema, ananiambia haya endelea na kama hakifai au ana majibu yake alikuwa anainiambia nisiulize,” amesema.

Chilolo amesema Lowassa atakumbukwa kwa mengi, ikiwemo ujenzi wa shule za sekondari za kata ambazo zimekuwa msaada kwa wanafunzi wanaofaulu. Awali, shule zilikuwa chache hivyo wanafunzi wengi walikuwa wanaachwa hata kama wamefaulu.

Amesema ujenzi wa zahanati kwa kila kata pia umesaidia kupunguza vifo vya wajawazito na watoto wachanga kwa kuwa wanapata huduma ya kujifungua jirani na maeneo wanayoishi.

Chilolo amesema zamani wajawazito walikuwa wanabebwa kwenye mikokoteni inayovutwa na ng’ombe, baiskeli na bodaboda kufuata huduma za afya mbali. Amesema Lowassa alikuwa mchapakazi na kwamba, kwa kiasi kikubwa alimsaidia Rais Jakaya Kikwete kutekeleza majukumu yake ya urais.

Kauli ya Msindai Aliyekuwa mbunge wa  Iramba Mashariki, Mgana Msindai ambaye kwa sasa amehamishia makazi yake mkoani Mwanza, amesema hakuna mtu anayeweza kupinga kifo ni lazima  wakubaliane na ukweli, licha ya kuachiwa masikitiko.

Msindai amesema Lowassa alikuwa rafiki yake na aliamua kuambatana naye kutokana na misimamo aliyokuwa nayo alipoamua kufanya jambo.

“Huyu bwana alikuwa akiamua kufanya jambo lake ni lazima alitimize, alikuwa si mtu wa kukata tamaa kirahisi na ndiyo maana wakati wa ujenzi wa shule za kata nchini kuna watu walikuwa wanambeza kuona kuwa azma hiyo haitafanikiwa, lakini matokeo yanaonyesha alifanikiwa kwa kiasi kikubwa,” amesema Msindai.

Amesema Lowassa alianzisha mambo mengi ambayo yamefanikiwa kwa kiwango kikubwa na kuacha alama ambazo si rahisi kufutika.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live
Related Articles: