Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Shein, Sumaye waeleza uchapakazi wa Lowassa

Shein Msiban.png Shein, Sumaye waeleza uchapakazi wa Lowassa

Tue, 13 Feb 2024 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Waziri Mkuu mstaafu, Frederick Sumaye amemtaja hayati Edward Lowassa kama kiongozi aliyeacha alama nyingi katika maisha yake hapa duniani, hivyo ataendelea kukumbukwa.

Lowassa aliyefariki dunia Februari 10, 2024 amehudumu katika nafasi mbalimbali za Chama cha Mapinduzi (CCM) na Serikali ikiwamo ya Waziri Mkuu kuanzia mwaka 2005 hadi 2008.

Akizungumza leo Februari 13, 2024 katika viwanja vya Karimjee, Sumaye amesema, “Kifo ni hatua ya mwisho maishani, kila mwanandamu na sote lazima tutapitia huko. Jambo muhimu katika maisha, je utakapokufa umeacha nini nyuma ambacho watu watakukumbuka?

“Lowassa ameacha mengi ambayo tutayakumbuka, amefanya kazi kwenye chama, serikali na mengi ameyafanya kwenye jamii, hivyo wanajamii wataendelea kumkumbuka.”

Sumaye amesema Lowassa alikuwa mchapakazi na aliyetekeleza majukumu yote aliyokabidhiwa.

Kwa upande wake, Rais mstaafu wa Zanzibar, Dk Ali Mohamed Shein amesema Lowassa alikuwa mchapakazi ambaye hakupenda kuzungumza maneno mengi.

“Lowassa siku zote nilikuwa nikimpa nafasi ya kusema, alisema nitasema kwa ufupi, nilivutiwa na hili na mimi leo nitasema kwa ufupi. Wengi tumefanya kazi na Lowassa, nimemfahamu kwa weledi, uchapakazi, heshima yake kwenye kazi na jinsi alivyojitoa.

“Mauti hayaepukiki, ila lazima tujiandae nayo ili yanapokuja yatukute tukiwa tayari, Lowassa alikuwa ananivutia alipokuwa serikalini kwa utendaji wake, ushupavu na weledi wake,” amesema Dk Shein.

Watanzania watakiwa kushukuru

Kwa upande wake, Mchungaji Joseph Mlaki kutoka Kanisa la Kiinjili la Kilitheri Tanzania (KKKT) Usharika wa Azania Front, alipokuwa akihubiri katika ibada ya maombolezo ya msiba wa kiongozi huyo, amesoma maandiko katika kitabu cha 1Wathesalonike 5:16-23 akisema "Furahini siku zote; ombeni bila kukoma; shukuruni kwa kila jambo; maana hayo ni mapenzi ya Mungu kwenu katika Kristo Yesu.

"Neno linasema furahini siku zote, lakini itasema nitafurahije siku zote, tunapaswa kufurahi kwa kuwa hayo ni mapenzi ya Mungu," amesema Mchungaji Mlaki.

Kuhusu kumwomba Mungu, amesema waumini wanapaswa kumuomba Mungu siku zote sawa na mapenzi yake.

"Tunapaswa kumshukuru Mungu siku zote kwa sababu ni mapenzi ya Mungu. Kumbuka safari ya maisha yako tangu ulipozaliwa hatari ambazo amekuepushia," amesema.

Akimzungumzia marehemu Lowassa, Mchungaji Mlaki amesema amevipiga vita na imani ameilinda.

"Mwili wake utakapopumzishwa roho yake imepumzishwa," amesema.

Amesema Lowassa aliyekuwa mshirika wa Kanisa hilo alipenda ibada na hata kama alikatisha ibada, alitoa taarifa kwamba ana mkutano au safari.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live
Related Articles: