Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

TV

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Richmond ilivyomwandama Lowassa

Lowassa Deaddd).jpeg Richmond ilivyomwandama Lowassa

Mon, 12 Feb 2024 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Mwaka 2008 Serikali ilitoa zabuni ya kufua umeme wa dharura kwa Kampuni ya Richmond Development Company LLC . Gharama ya zabuni hiyo ilikuwa Sh172 bilioni.

Serikali kupitia Shirika la Umeme (Tanesco), ilitoa zabuni hiyo na mkataba ukafikiwa kati ya pande mbili, kutokana na Taifa kukumbwa na upungufu mkubwa wa umeme mwaka 2006, hali iliyoilazimu Serikali kuagiza mitambo kwa ajili ya kufua umeme wa dharura.

Hata hivyo, kukodishwa mitambo ya kufua umeme kutoka Richmond, ilibainika baadaye kuwa ni mkataba wa kifisadi na iliundwa Kamati ya Bunge iliyoongozwa na Dk Harrison Mwakyembe kuchunguza na ripoti yake kutolewa bungeni, ikihusisha ofisi ya Waziri Mkuu, Edward Lowassa aliyelazimika kujiuzulu wadhifa huo.

Kujiuzulu Lowassa

Februari 7, 2008, wakati wa mjadala wa taarifa ya Kamati Teule ya Bunge iliyochunguza mchakato wa zabuni ya kuzalisha umeme wa dharura ulioipa ushindi Richmond Development Company LLC ya Huston, Texas, Marekani mwaka 2006, Lowassa alisimama bungeni na kusema yafuatayo:

"Mheshimiwa Spika, kwanza napenda kuchukua nafasi hii kukushukuru sana kwa kunifanya msemaji wa kwanza katika hoja hii.

Lakini la pili, nimpongeze Dk Harrison Mwakyembe, Mwenyekiti wa kamati Teule kwa kuwasilisha kwa mbwembwe nyingi sana taarifa yake, mbwembwe zilikuwa nzuri kweli.

Kwa kazi nzuri, kwa maoni yao, wamewasilisha vizuri. Lakini, nimesimama kuweka kwenye kumbukumbu kutoridhika kwangu na jinsi kazi hiyo ilivyofanywa.

Mheshimiwa Dk Mwakyembe ni mwanasheria, tena daktari alikuwa anafundisha chuo kikuu. Moja ya vitu alivyokuwa anafundisha ni ‘Natural Justice’ (haki asili).

Mheshimiwa Spika, wewe ni mwanasheria unafahamu suala la Natural Justice. Kwamba, Kamati Teule imesikiliza watu wengine wote pamoja na wanaoita minong'ono ya mitaani, wamesafiri mpaka Marekani kutafuta mashahidi, lakini mimi ambaye ni mmoja kati ya watuhumiwa mle hawakunihoji hata siku moja.

Mheshimiwa Spika, nimesimama kueleza masikitiko yangu. Ofisi ya Bunge mpaka ofisini kwangu hata kama wangeniita ningeenda kwa miguu kama hamna gari na nilikuwa tayari kufanya hivyo. Hawa ni watu makini sana siwezi kuamini kwamba wanaweza wakafanya ‘oversite’ kama hiyo.

Kwa sababu katika kila hoja walizojenga wamesema Waziri Mkuu ilikuwa hivi. Kulikuwa na shida gani kuja kuniuliza Waziri Mkuu wanasema ulitoa dokezo hili ni sawasawa kweli?

Kulikuwa na shida gani kwa mfano kufuata utaratibu wa Westminster kuthibitisha hapo unaposema mwenye Richmond ni fulani uka-lay on the table records na ushahidi kuwa ni fulani.

Mheshimiwa Spika, Taifa letu ni Taifa changa, lakini chombo hiki ndiyo mahali pa demokrasia pakubwa katika nchi yote, hapa ndipo penyewe. Kama katika chombo hiki haki haitaonekana kutendeka nchi yetu haitakwenda vizuri.

Hapa ndipo tunategemea tuwaonyeshe umakini wetu, umahiri wetu katika mambo ya demokrasia. Kwa hiyo, nilichofanyiwa napenda kuweka kumbukumbu sawa kwamba naona si sahihi, nimefadhaika sana, nimedhalilishwa sana, nimeonewa sana katika hili.

Maana zimechukuliwa tuhuma zikaelezwa hapa kwamba hivi ndivyo ilivyo. Mimi sijauliza. Kulikuwa na shida gani kuniuliza, kwa nini muamini minong'ono ya mitaani kuliko maelezo yangu. Sisi wote hapa ni wanasiasa tukianza kuamini minong'ono ya mitaani niambieni mwanasiasa atakayesimama. Hatuwezi, tume imepewa muda wa kutosha lakini inashindwa kumuona mtu ambaye wanamtuhumu na wanamsema kwa kirefu sana.

Mheshimiwa Spika, lakini hata pale uliponinong'oneza ukaniambia una ushahidi wowote? Nilikupa ushahidi huo wa maandishi. Katika taarifa yao hakuna hata moja ya ushahidi ambao umetoka kwa Waziri Mkuu. Kile kitabu cha majedwali kimejaa majedwali mengi pamoja na magazeti mpaka ya udaku lakini maelezo ya Waziri Mkuu hakuna hata moja.

Mheshimiwa Spika, naamini ingekuwa ni heshima wangeiweka halafu wakasema tunakataa kitambulisho hiki kwa sababu hii na hii, hiyo ndiyo imejengwa hoja. Lakini kujenga hoja na kuja hapa bungeni tunahutubia nchi nzima na kusema Waziri Mkuu amefanya hiki, amefanya hiki bila ya kumsikiliza nachelea kuuliza hivi mtu wa chini itakuwaje?

Mheshimiwa Spika, lakini nimetafakari kwa makini sana jambo hili nikajiuliza hivi kulikoni mpaka watu wazima wenye uwezo wao, watu maarufu wenye heshima zao, mpaka wafike mahali waache jambo la msingi kama hilo kulikoni? Mimi nadhani there is a wish which I am going to grant, ni Uwaziri Mkuu. Nadhani tatizo ni Uwaziri Mkuu. Kwamba ionekane Waziri Mkuu ndiyo amefanya haya, tumuondolee heshima au tumwajibishe.

Mheshimiwa Spika, nimetafakari kwa niaba ya chama changu, kwa niaba ya Serikali yangu nimeamua kumwandikia Rais barua ya kumwomba niachie ngazi. Nafanya hivyo kwa moyo mweupe kabisa ili kuonyesha dhana ya uwajibikaji lakini kutokubaliana na utaratibu uliotumika kusema uongo ndani ya Bunge wa kumsingizia mtu.

Mheshimiwa Spika, nitumie nafasi hii kumshukuru sana Rais kwa heshima aliyonipa ya kutumikia nchi hii kwa uwaziri mkuu kwa miaka miwili.

Namshukuru sana Mheshimiwa Rais. Nakushukuru wewe, nawashukuru mawaziri na naibu mawaziri, nawashukuru waheshimiwa wabunge na wanachama wa CCM tuliosimamia ilani ya uchaguzi ya Chama cha Mapinduzi,” mwisho wa nukuu ya Lowassa.

Kikwete kuhusu Richmond

Wakati wa kampeni za uchaguzi mkuu wa mwaka 2015, katika moja ya mikutano ya CCM, Kikwete akihutubia hadhara alisema kama ifuatavyo kuhusu Richmond:

“Tulitambua pamoja tatizo kubwa linalowasumbua Watanzania linalowapa chuki ni suala la rushwa, tukasema hatutaki mgombea mwenye makandokando ya rushwa.

Sasa hivi wana kazi kubwa ya kumtetea, Richmond sio yeye, sio yeye eti Richmond ni ya Kikwete, ni uongo mtupu. Jana Mwakyembe (Harrison) alieleza vizuri.

Tatizo kwenye Richmond tulikubaliana kweli, mabwawa yetu yamekauka tukodishe mitambo nje ya kuzalisha umeme, hili tumekubaliana wote na mimi nimehusika. Mimi sijahusika ni kampuni gani ilete hiyo mitambo.

Na kwenye kikao cha Baraza la Mawaziri tulipokuwa tunajadili nilieleza wazi kanuni za manunuzi ziheshimiwe. Tatizo kwenye Richmond kanuni hazikuzingatiwa.

La kwanza lillilovunjwa, badala ya shughuli hiyo ifanywe na Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco) Waziri Mkuu aliunda kamati ya makatibu wakuu ifanye kazi hiyo, inatoa taarifa kwa waziri mkuu ndiyo maana Kamati ya Bunge ikamwambia wewe mzee ndiyo chanzo cha tatizo hili.

Matokeo yake ikapatikana kampuni isiyo na uwezo wa kutimiza huo wajibu nchi ikawa kwenye mgogoro, wawe wakweli tu.

Tundu Lissu siku moja akaniuliza nikamwambia usiniulize mimi mwenye Richmond unaye wewe.

Kuamua kwamba tupate mitambo ya kuzalisha umeme hili nimeshiriki kuamua, lakini sijashiriki kuamua kampuni ya kuzalisha huo umeme iwe Richmond. Maagizo yangu yalikuwa taratibu za manunuzi zizingatiwe, imekiukwa ndiyo sababu ya mgogoro huu.

Mgogoro mpaka ulipotufikisha hapo tulipofikia na kumwambia bwana mkubwa jiuzulu tuunde upya Serikali, kama Richmond ingekuwa ni yangu aliyewahi kuwa Waziri wa Nishati Msabaha (Ibrahim) alishakuja kwangu akiwalalamikia watu wa Wizara ya Fedha kwamba Rais nisaidie wamekataa kutoa fedha za awali kwa ajili ya kampuni kuleta mitambo.

Mimi nilimwambia nawaunga mkono Wizara ya Fedha, nilimwambia Waziri hii kampuni ni hewa hawa ukiwapa hizo pesa wataondoka na hiyo Dola milioni 10 wataondoka nayo na mitambo hutaiona.

Nikamwambia hapana, kama wana uwezo wa kuleta mitambo walete hiyo Dola milioni 10 watapewa hawakuweza kuleta, ndiyo nchi ikapata matatizo kama ni kampuni yangu si ningejilipa, ningezuia kweli wasilipwe maneno hayana kichwa wala miguu, limewakwama kooni kama kijiba cha samaki.’’

Agoma kujibu swali la Richmond

Hata hivyo, kwenye kampeni hizohizo za mwaka 2015, Lowassa alikataa kujibu swali lililomtaka aeleze kilichotokea kwenye sakata la Richmond, akisema swali hilo “halina maana”.

Katika moja ya mikutano, Septemba 11, 2015, Lowassa aliamua kutohutubia na badala yake aliruhusu wananchi wamuulize maswali alipokuwa katika Kijiji cha Mvumi, Wilaya ya Chamwino mkoani Dodoma.

Baada ya kutoa nafasi kwa wananchi kuuliza maswali, Michael Makanyi alitaka kufahamu kama Lowassa, ambaye anagombea urais kwa tiketi ya Chadema, anahusika katika sakata hilo linalohusu kuipa Richmond Development Company ya Marekani zabuni ya kufua umeme wa dharura wakati nchi ilipokumbwa na tatizo la ukosefu wa nishati hiyo mwaka 2006.

“Ulipokuwa Waziri Mkuu ulijenga hospitali ngapi, wewe unatuhumiwa katika Richmond na tatu Wamasai wamekuwa na tabia ya kufanya vurugu na kuingiza mifugo katika mashamba ya wakulima. Sasa kama umeshindwa kuwatuliza Wamasai huko kwenu, utaweza kumaliza vipi migogoro ya ardhi?” aliuliza Makanyi kwenye mkutano huo uliofanyika Uwanja wa Shule ya Msingi Mvumi kwenye Jimbo la Mtera ambalo ni ngome ya CCM.

Akijibu maswali hayo, Lowassa, alisema: “Maswali yako mawili ya mwisho hayana maana (swali la Richmond na Wamasai), ila la kwanza najibu. Ilani ya CCM ilikuwa ikizungumzia afya na elimu, lakini tulianza na elimu. Tulijenga shule katika kila kata.”

Chanzo: www.tanzaniaweb.live
Related Articles: