Rais Samia Suluhu Hassan, anatarajiwa kuongoza waombolezaji katika maziko ya Waziri Mkuu wa zamani, Edward Lowassa yanayotarajiwa kufanyika wilayani Monduli Mkoa wa Arusha, Jumamosi Februari 17, 2024.
Juzi, Februari 10, 2024 baada ya Makamu wa Rais, Dk Philip Mpango kutangaza kifo cha Lowassa, Rais Samia alitangaza siku tano za maombolezo ya kitaifa ambapo bendera zitapepea nusu mlingoti kuanzia jana.
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa leo Jumapili, Februari 11, 2024 akitoa taarifa ya ratiba ya mazishi ya kiongozi huyo, amesema katika kipindi cha maombolezo, Taifa litaendelea na shughuli za umma na kijamii sambamba na kushirikiana na wanafamilia katika ratiba ya msiba kama ilivyoandaliwa na kamati ya mazishi ya kitaifa na wanafamilia.
Amesema kabla ya maziko, mwili wa Lowassa unatarajiwa kuagwa katika viwanja vya Karimjee, jijini Dar es Salaam na Sheikh Amri Abeid, jijini Arusha.
Majaliwa amesema Jumanne Februari 13, 2024 mwili wa kiongozi huyo utaagwa na viongozi na wananchi katika viwanja vya Karimjee.
Jumatano Februari 14, utapelekwa katika Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), Azania Front kwa ajili ya ibada ambako pia utaagwa.
Amesema Alhamisi Februari 15, utasafirishwa hadi jijini Arusha ambapo viongozi na wananchi watapa fursa ya kuaga katika viwanja vya Sheikh Amri Abeid.
Alichosema Mbowe
Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe amesema Lowassa ni miongoni mwa viongozi waliostahili kushika nafasi za juu za uongozi nchini.
Amesema hilo halikutokea kutokana na kile alichoeleza kwamba Watanzania wamekuwa na tabia ya kuona umakini na uhalisia wa mtu pale itakapotokea hayupo duniani.
Mbowe ametoa kauli hiyo alipofika nyumbani kwa Lowassa Masaki jijini Dar es Salaam, leo Februari 11, 2024.
Mbowe amesema mwanasiasa huyo alikuwa kiongozi mahiri na alistahili kuwaongoza Watanzania kutokana na umahiri wake.
“Alikuwa kiongozi makini, aliwaunganisha watu wengi na aligusa watu wengi katika maisha yake ya kawaida na kiuongozi.
“Unaona kabisa alipaswa kuwa kiongozi mkubwa wa Taifa hili, bahati mbaya hatujamtumia sana haya mengine yaliyotokea ni bahati mbaya,” amesema.
Kumfahamu kwake Lowassa, amesema kumetokana na kipindi ambacho mwanasiasa huyo alikuwa mgombea urais wa Chadema na Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa) katika Uchaguzi Mkuu 2015.
Mbali na kufanya naye kazi kipindi hicho, amesema amemfahamu zaidi alipokuwa mmoja wa wajumbe wa Kamati Kuu ya Chadema baada ya uchaguzi huo.
“Nimefanya naye kazi kwa karibu akiwa mgombea wa urais wa chama chetu na baadaye alihudumu kama mjumbe wa Kamati Kuu ya Chadema,” amesema.
Julai 2015, Lowassa alitangaza kujiunga na Chadema, akitokea CCM siku chache baada ya chama chake hicho kukata jina lake katika kinyang'anyiro cha kuwania urais.
Lowassa alikuwa miongoni mwa makada wa CCM waliotangaza nia ya kuwania urais katika uchaguzi mkuu wa mwaka 2015 na jina lake lilikatwa mapema, huku Dk John Magufuli akipewa jukumu la kupeperusha bendera ya CCM katika kinyang'anyiro hicho.
Uamuzi huo wa CCM ulimfanya mwanasiasa huyo kutafuta jukwaa lingine la kuwania urais na Julai 28, 2015 alitangaza kujiunga na Chadema.
Hatua hiyo ilifufua nguvu ya siasa za upinzani na kusababisha ushindani mkubwa katika uchaguzi huo, ukizingatia vyama vya upinzani viliungana kuunda Ukawa.
Kutokana na ushawishi aliokuwa nao, katika uchaguzi huo, Lowassa alipata kura milioni 6.07 dhidi ya kura milioni 8.8 alizopata Dk Magufuli na kushinda.
Kura hizo zilikuwa nyingi zaidi kwa mgombea urais wa upinzani kuwahi kupata tangu mfumo wa siasa za vyama vingi uanze nchini.
- Kisa cha Diana Chilolo kufuta namba ya Lowassa
- Tazama hapa msafara wa mwili wa Lowassa ukipelekwa Karimjee
- Shein, Sumaye waeleza uchapakazi wa Lowassa
- Picha: Matukio mbalimbali katika zoezi la kuaga mwili wa Lowassa
- Fredy Lowassa: Asingekuwa Rais Samia, baba asingefika juzi
- Read all related articles