Mpwa wa aliyekuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Hayati Dkt. John Pombe Magufuli aitwaye Furaha Dominiki amefunguka namna ambavyo alipambana mpaka kupata ushindi wa kishindo katika kura za maoni za wajumbe ndani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) wakati wa mchakato wa uchaguzi Mkuu wa mwaka 2020.
Furaha amesema yeye hakuwa na pesa kama watu ambavyo wamekuwa wakisema bali alijikita katika kueleza sera zenye mrengo wa kutatua changamoto za wananchi wa Jimbo la Kawe alilokuwa akiwania Ubunge.
“Nilikuwa nikiwaambia akija mtu akakuuliza Furaha ametoa ngapi mwambie hata milioni, kwa kiongozi anayeamini kupata dhamana ni kutoa pesa atatoa, lakini mimi nilijikita kueleza sera ambazo zingetatua changamoto za wananchi wa Kawe.
“Sera zangu zilikuwa zaidi ya pesa, sikuwa na umaarufu mitandaoni lakini niliwazidi wengi ambao walikuwa na majina na walikuwa na pesa. Wanaosema waache waseme lakini Wanakawe wanajua kama mimi nilijikita katika hilo na si vinginevyo.
“Wengine walidhani nimepata kura nyingi kuliko wote kwa sababu ya udugu wangu na Magufuli, lakini mimi sikuwahi kusema popote kuanzia shule mpaka kwenye utumishi wangu, mpaka yeye alipokuja kusema kwa mdomo wake kwamba mimi ni mtoto wa dada yake,” amesema Furaha.