Mpwa wa aliyekuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Hayati Dkt. John Pombe Magufuli aitwaye Furaha Dominic amesema bado ana mpango wa kurejea katika siasa na kuwania ubunge wa Jimbo la Kawe.
Kijana huyo aliongoza katika kura za maoni Kawe kwenye uchaguzi mkuu wa mwaka 2020 licha ya chama chake CCM kutopitisha jina lake na badala yake kupitishwa Askofu Josephat Gwajima ambaye ndiye mbunge wa sasa wa Jimbo hilo.
Furaha amesema hayo wakati akifanya mahojiano na Global TV Online katika kipindi maalum cha Hoja kwa Hoja na kuongeza kuwa licha ya familia yake kutotaka afanye mambo ya siasa lakini yeye kama kijana anawiwa kuwatumikia wananchi hao hivyo mpango wake hautakoma mpaka afanikiwe.
"Mimi ni kijana mdogo bado, na ni Taifa la kesho na nitaitetea katiba ya nchi yangu na kulilinda Taifa langu na kuwatetea watu wangu.
"Mpango wa kutafuta uongozi hauwezi kukoma kama una spirit ya kuwasaidia watu, mpaka sasa bado ninaendelea. Nitanukuu maneno ya Rais wangu Samia Suluhu alisema, ‘nani aliwaambia kwamba sigombei 2025?’
"Na mimi ukiniuliza nikakataa kwamba sitagomea mwaka 2025 nitakuwa mnafiki kwa Mungu, aliyepewa dhamana ya Kawe (Askofu Josephat Gwajima) anatakiwa atambue mimi nipo, aangalie yale aliyopaswa kuyafanya (jimboni) amefanya?
"Lakini ajue nipo ninapiga jaramba. Mimi nilichaguliwa na wananchi, mimi naweza nisitake lakini dhamira yao ipo wananihitaji, kwa hiyo mimi nipo na nitakuwepo," amesema Furaha.