Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Msimamo wa Lowassa unavyowakuna viongozi

Lowassa X Mke X Samia Msimamo wa Lowassa unavyowakuna viongozi

Sun, 11 Feb 2024 Chanzo: Mwananchi

Kufuatia kifo cha Waziri Mkuu wa zamani, Edward Lowassa, baadhi ya viongozi na wanasiasa wameomboleza wakikumbuka walivyofanya kazi naye na mchango wake kwa Taifa.

Taarifa iliyotolewa na Makamu wa Rais Dk Philip Mpango alipotangaza msiba huo kupitia televisheni ya Shirika la Utangazaji la Taifa (TBC) leo Februari 10,2024 imesema Lowassa amefariki baada ya kuugua magonjwa ya kujikunja utumbo, matatizo ya mapafu na shinikizo la damu.

Rais Samia Suluhu Hassan ni miongoni mwa viongozi waliomlilia Lowassa kupitia ukurasa wake wa X akieleza masikitiko yake kwa msiba huo.

“Mheshimiwa Lowassa ameitumikia nchi yetu katika nafasi mbalimbali kwa zaidi ya miaka 35, akianzia ushiriki wake katika Jeshi la Wananchi wa Tanzania, Chama Cha Mapinduzi (CCM), Mbunge, Waziri katika wizara mbalimbali na Waziri Mkuu.

“Tumempoteza kiongozi mahiri, aliyejituma na kujitoa kwa nchi yetu. Natoa pole kwa mjane, Mama Regina Lowassa, watoto (Mheshimiwa Mbunge wa Monduli, Fredrick Lowassa na wadogo zako), ndugu, jamaa, marafiki na Watanzania wote kwa msiba huu mzito.”

Rais Samia amewaeleza kuwa kama Taifa wako pamoja nao katika kipindi hiki kigumu.

“Kamwe wasiache kumtegemea Mwenyezi Mungu na kutafakari neno lake, hasa Kitabu cha Ayubu 1:21.”

Sumaye amlilia

Lowassa aliteuliwa kuwa Waziri Mkuu na Rais wa awamu ya nne, Jakaya Kikwete baada ya uchaguzi mkuu wa 2005, akirithi kiti hicho kutoka kwa mtangulizi wake, Frederick Sumaye.

Akizungumza jana na Mwananchi, Sumaye amesema hakumfahamu Lowassa baada ya kumwachia kiti cha wadhifa huo, bali walifahamiana kabla.

Ameeleza wawili hao walifahamiana pale Sumaye alipokuwa Waziri Mkuu na Lowassa akiwa aziri wa wizara mbalimbali katika Serikali ya awamu ya tatu.

“Nilipokuwa Waziri Mkuu alikuwa (Lowassa) waziri katika Serikali ya awamu ya tatu na alikuwa mchapakazi na mwenye uamuzi. Jambo hata kama ni gumu anaweza kulifanyia uamuzi katika wizara yake,” amesema.

Ameeleza ni kiongozi aliyetegemewa zaidi katika utendaji wake na kwa hatua aliyofikia ni vema kila Mtanzania amtakie mapumziko mema.

Kuhusu kumwachia kiti cha uwaziri mkuu, Sumaye alisema alimkabidhi mwanasiasa huyo nyaraka zote zinazostahili na walizungumza mambo mengi.

“Siwezi kueleza mambo tuliyozungumza kwa sababu ni ya ndani sana, lakini tulikabidhiana nyaraka zote,” amesema.

Mgeja akumbuka uvumilivu

Katika harakati za kuusaka urais ndani ya CCM mwaka 2015, Lowassa alifanya kazi kwa karibu na viongozi wa chama hicho wakiwamo wenyeviti wa mikoa, na kiongozi wao wakati huo ni aliyekuwa Mwenyekiti wa Mkoa wa Shinyanga Hamisi Mgeja.

Akizungumza kwa simu na Mwananchi jana, Mgeja ameeleza ukaribu wake na Lowassa akisema amejifunza mengi.

“Tulikuwa karibu sana katika masuala ya siasa, kwa kweli tumeondokewa na kiongozi makini, mpole na mvumilivu.

“Nakumbuka wakati wa uchaguzi wa 2015, baada ya hayati John Magufuli kutangazwa kuwa mshindi, vijana ambao hawakuridhishwa na matokeo yale, walikusanyika wakamwambia tunasubiri ruhusa yako tuingie barabarani.”

“Lakini yeye kwa busara zake akawaambia wavumilie kwa matokeo yale na kwamba hayuko tayari kuingia Ikulu mikono ikiwa imejaa damu,” amesema.

Akifafanua kuhusu uvumilivu wa Lowassa, Mgeja amesema: “Alitukanwa na alibezwa na kuna watu walipandishwa vyeo kwa sababu ya kumtukana, lakini hakuwajibu, bali alisema wasameheni kwa kuwa hawajui watendalo.”

Alikumbusha suala la Lowassa kujiuzulu mwaka 2008, akisema alionyesha uwajibikaji kwa jambo ambalo hakulifanya.

Sofia Simba

Kiongozi mwingine aliyekuwa karibu na Lowassa alikuwa Mwenyekiti wa Umoja wa Wanawake wa CCM (UWT), Sofia Simba.

Akizungumza na Mwananchi jana, Simba amesema anamkumbuka Lowassa kwa mchango wake kwa Taifa katika nyadhifa alizofanyia kazi.

“Mchango wake kwa Taifa ulikuwa ni mkubwa na kwa kweli alikuwa mpiganaji. Nakumbuka nilipokuwa nikifanya kazi chini yake, alikuwa akipita kutuelekeza, alikuwa mwalimu mzuri,” amesema.

Simba aliyefukuzwa uanachama wa CCM mwaka 2017 pamoja na viongozi mbalimbali wa chama hicho kwa masuala ya nidhamu.

Hata hivyo, ameelezwa kilichowaponza ni kumuunga mkono Lowassa katika harakati zake za kuwania urais ndani ya CCM.

Mbali na Simba, CCM ilimsamehe Adam Kimbisa ambaye ni Mwenyekiti chama hicho Mkoa wa Dodoma na kilimpa onyo kali Emmanuel Nchimbi ambaye sasa ni Katibu mkuu wa chama hicho.

Wengine waliofukuzwa uanachama ni waliokuwa wenyeviti wa chama hicho wa mikoa, akiwamo Ramadhani Madabida (Dar es Salaam), Jesca Msambatavangu (Iringa), Erasto Kwilasa (Shinyanga) na Christopher Sanya (Mara) na aliyekuwa Mwenyekiti wa UWT Mkoa wa Kigoma, Josephine Genzabuke amepewa onyo kali.

Alipoulizwa leo kuhusu sakata hilo, Simba ambaye sasa amerudi CCM hakutaka kuingia kwa undani.

“Hayo ya uchaguzi naona siyo vizuri kuyazungumza kwa sasa, ni sehemu ya siasa.”

Zitto amkumbuka kwa kujiuzulu

Kiongozi wa ACT Wazalendo, Zitto Kabwe naye amemlilia Lowassa akikumbuka uamuzi aliouchukua Lowassa alipokuwa madarakani.

“Mchango wake katika kuimarisha demokrasia ya vyama vingi ulikuwa mkubwa. Utayari wake wa maamuzi bado unaonekana (shule za sekondari za kata na utekelezaji wa uamuzi wa kuanzisha chuo Kikuu cha Dodoma).

“Ni mwafaka kabisa ukumbi mkubwa wa mikutano wa Chuo Kikuu cha Dodoma uitwe Edward Lowassa Chimwaga Hall kuenzi msimamo wake thabiti wa kusimamia maelekezo ya kuanzishwa chuo kile,” amesema.

Naye Waziri wa Fedha, Dk Mwigulu Nchemba ameandika katika ukurasa wake wa X akisema, “Tutamkumbuka kwa mchango wake mkubwa aliotoa kwa maendeleo ya Taifa letu. Natoa pole zangu nyingi kwa familia, ndugu, jamaa na marafiki.”

Nape na harakati za Lowassa

Mwanasiasa anayekiri kutofautiana na Lowassa kisiasa ni Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Nape Nnauye.

Katika ukurasa wake wa X, ameweka nukuu ya maneno Lowassa aliyoyatoa walipokutana baada ya uchaguzi wa 2015.

“Nape, tumepishana kwenye siasa, lakini napenda mtu anayesimamia anachoamini hasa kwa umri wenu,” ameandika Nape akiipa pole familia ya Lowassa.

Naye wakili maarufu John Mallya, amesema alimfahamu Edward Lowassa kama mmoja wa wanasiasa wenye uthubutu zaidi kuwahi kutokea hapa nchini Tanzania.

“Alikuwa mpenda mabadiliko aliyeipenda nchi yake, Lowassa alichukia unyonge na umasikini kwa vitendo.

“Alipenda zaidi siasa za vitendo kuliko maneno. Daima aliamini kwamba elimu ndio ukombozi sahihi wa Taifa la Tanzania,” amesema.

Chanzo: Mwananchi
Related Articles: