Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Madaktari wachambua magonjwa yaliyosababisha kifo cha Lowassa

 102258880 905c91c5 314f 42ce A5b2 D177649b5660 Madaktari wachambua magonjwa yaliyosababisha kifo cha Lowassa

Sat, 10 Feb 2024 Chanzo: Mwananchi

Baadhi ya madaktari wamezungumzia kitaalamu magonjwa ambayo yanatajwa kusababisha mauti ya Waziri Mkuu wa zamani, Edward Lowassa (70) aliyefariki leo Februari 10, 2024.

Kwa mujibu wa Makamu wa Rais, Dk Philip Mpango, wakati akitangaza kifo cha Lowassa alisema amefariki wakati akiendelea na matibabu ya magonjwa ya kujikunja utumbo, matatizo ya mapafu na shinikizo la damu.

Daktari bingwa wa magonjwa ya mfumo wa upumuaji na magonjwa ya ndani, Dk Elisha Osati amesema utumbo kujikunja ni kitu cha tofauti, hakina uhusiano wa moja kwa moja na shinikizo la damu wala mapafu.

Amesema utumbo kujikunja maana yake ni sehemu ya tumbo na sanasana utumbo mwembamba ambapo chakula hakiwezi kupenya kirahisi.

“Mtu anapoumwa ugonjwa huo choo hushindwa kupita, chakula na wakati mwingine hewa haipiti mfano mtu hawezi hata kujamba,” amesema Dk Osati.

Akieleza sababu za kutokea hali hiyo, daktari huyo amesema zipo nyingi na mara nyingine mtu anaweza akawa amefanyiwa upasuaji zamani ambapo hutengeneza makovu tumboni au baadhi ya wenye saratani pia hupata shida hiyo.

Sababu nyingine ameeleza kuwa ni kama mtu amemeza kitu kisicho chakula, ambacho hakimeng’enyeki, hivyo hapati choo kwa muda mrefu hali ambayo huwapata zaidi wagonjwa wa sukari.

“Kwa hiyo ni vitu vingi vimehusianishwa na inaweza kumpata mtu wa umri wowote,” amesema.

Hata hivyo Dk Osati amesema endapo utumbo ukijikunja, mtu akiwahi anaweza kufanyiwa upasuaji.

Pia amefafanua kuwa utumbo unapojikunja maumivu yanakuwa makali ambapo madini ya potassium na sodiam yanapanda sana kwenye mwili na mwathirika anaweza kupata upungufu wa maji.

Kuhusu mapafu

Dk Osati amesema mtu anapokuwa na matatizo ya mapafu, japo hajajua Lowassa alikuwa anasumbuliwa na ugonjwa gani haswa, inaweza ikawa labda amepata maambukizi.

Amesema hii ni rahisi kumpata mgonjwa ambaye amelala au mtu mzima ambaye ana umri wa uzee kama Mzee Lowassa.

“Kwa umri wa Lowasa ni rahisi kupata magonjwa ya mapafu kwani kinga za mapafu huwa zinakuwa zimetetereka kidogo.”

“Ukizingatia pia alikuwa ana shida ya pressure (shinikizo la damu) ambayo nayo huathiri mfumo wa moyo na mapafu, kwa hiyo inaweza kuwa ni chanzo cha tatizo,” amesema Dk Osati.

Naye Daktari bingwa wa upasuaji kutoka Hospitali ya Taifa Muhimbili na Rais Mteule wa Chama cha Madaktari, Mugisha Nkoronko amesema utumbo kujikunja ni moja ya magonjwa hatari yanayowapata binadamu.

Akifafanua zaidi, Dk Nkoronko amesema utumbo wa binadamu umegawanyika katika sehemu kuu mbili, yaani utumbo mdogo na utumbo mpana.

Amesema utumbo mpana umetembea na kunasa pande mbili za tumbo (pembeni pembeni), wakati utumbo mdogo umejaa katikati.

Hata hivyo Daktari huyu amesema utumbo una sehemu ambazo hujishika na sehemu ambazo haujajishika (yaani zipo huru). Sasa ile sehemu ambayo ipo huru inaweza ikazunguka na kujisokota.

Aidha amesema katika harakati za kusukuma chakula kutoka sehemu moja kwenda nyingine kwa sababu mbalimbali inaweza kusababisha eneo hilo kujikunja.

“Kwa hiyo utumbo mdogo kujikunja mara nyingi huwa unakuwa umeshikwa na kambakamba nyingi zilizojitengeneza ndani ya tumbo, na kusababisha kuingia sehemu kama mpira na ukashindwa kutoka,” amesema.

Kwa utumbo mpana, Dk Nkoronko amesema hutokea kwa watu ambao wanapata shida ya kupata haja kubwa.

“Hivyo ule msukumo wa kusukuma choo kigumu husababisha ile sehemu ambayo haijashikwa kuongezeka saizi na kuanza kuning’inia na ikishaning’inia huko ndani ya tumbo unaweza kujisokota.”

“Vitu vingine vinavyoweza kusababisha utumbo kujisokota ni pamoja na magonjwa ya minyoo, au kama mtu aliwahi kufanyiwa operesheni zamani, maumbile ya utumbo wake hayajajishika vizuri Aidha Daktari huyu amesema hali hii akitokea husababisha tumbo kujaa sehemu ambayo haijajishika na yale majimaji yanayotakiwa au uzito uliopo katikati ya utumbo hujaza tumbo na hatimaye mtu anaweza kusikia kutapika na tumbo kuuma, kutopata choo wala kujamba.

Amesema mgonjwa akifikia hatua hii anapaswa kupelekwa hospitalini mara moja, ambako hufanyiwa matibabu ya upasuaji.

Hata hivyo mtaalamu huyu alisema ugonjwa huu huwapata zaidi wanaume kuliko wanawake, huku walio hatarini zaidi ni wale ambao walishawahi kufanyiwa operesheni za tumbo bila kujali umri wao.

Chanzo: Mwananchi
Related Articles: