Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Kilichomsikitisha Lowassa miaka miwili nje ya CCM

Lowassa Edward Wasifu Waziri Mkuu Mstaafu wa Tanzania, Edward Lowassa

Sun, 11 Feb 2024 Chanzo: Mwananchi

Kifo cha Waziri Mkuu wa zamani, Edward Lowassa kilichotokea jana Februari 10, 2024 kimeibua kumbukumbu nyingi tofauti katika safari yake kisiasa na kimaisha.

Moja ya mambo ambayo yanazungumzwa kwenye mitandao ya kijamii ni safari yake ya matumaini, ya kuwania uraia aliyoihitimisha kwa kuhama CCM kwenda Chadema.

Hata hivyo, akiwa upinzani baada ya kushindwa urais na Dk John Magufuli, kabla ya uamuzi wa kurejea CCM, alieleza jambo moja lililokuwa linamuumiza, ingawa halikufanya ajutie uamuzi wake.

Alipozungumza na Mwananchi Julai 2017, ikiwa ni miaka miwili kamili baada ya kuihama CCM, Edward Lowassa alisema hajutii uamuzi wake, yuko imara na licha ya kuzuiwa kufanya mikutano, kura zake zinazidi kuongezeka.

Katika mazungumzo hayo, Lowassa alisema pamoja na kupata kura zaidi ya milioni sita za urais, yeye na wapinzani wenzake wanasononeshwa na kunyimwa haki ya kufanya mikutano na kukutana na wanachama wao.

Hata hivyo, alipoulizwa ni kwa kiwango gani kunyimwa fursa ya mikutano kumemuathiri, alisema: “Kura zangu zimeongezeka sana, tena sana. Ile tu kutoniona kunaniongezea (kura).

“Nataka kwenda kuwaona (wananchi) lakini siruhusiwi. Nataka kufanya mikutano ya hadhara, siruhusiwi. Si mimi tu, ni pamoja na wenzangu wote kwenye vyama vya upinzani, hii ndiyo kauli yao.

“Waeleze wananchi na wanachama wa Chadema, nawapenda sana. Natamani kwenda kwao, kuzungumza nao, lakini sipati nafasi.”

Alikuwa akizungumzia amri ya kuzuia mikutano ya hadhara ya wanasiasa iliyowekwa na Serikali. Zuio hilo lilifutwa na Rais Samia Suluhu Hassan Januari 2023.

Hana lolote la kujutia

Lowassa katika mazungumzo hayo na Mwananchi, wakati huo akiwa Mjumbe wa Kamati Kuu ya Chadema, alisema pamoja na hali hiyo wanayokumbana nayo wapinzani, hakuwa na cha kujutia kutokana na uamuzi wake wa kujiunga na upinzani.

“Sina cha kujutia hata kidogo,” alisema katika mahojiano hayo yaliyofanyika ofisini kwake jijini Dar es Salaam.

“Nadhani ulikuwa uamuzi sahihi. Baada ya kuutafakari wakati ule na sasa, bado naamini ulikuwa uamuzi sahihi.”

Pamoja na hayo, Lowassa aliyewania urais na kupata kura milioni 6.07 sawa na asilimia 39.97 dhidi ya Rais Dk John Magufuli aliyepata kura milioni 8.8 (asilimia 58.46), alisema kuna tofauti kubwa katika kufanya siasa ukiwa CCM na ukiwa upinzani.

Alisema hali ni tofauti kwa sababu kuna changamoto nyingi zaidi kwenye chama cha upinzani ukilinganisha na CCM.

Alisema kuna maswali mengi ambayo yanajitokeza na CCM ilikuwa na muundo na miundombinu ya kuyakabili mambo hayo, tofauti na ilivyo kwenye vyama vya upinzani kutokana na uchanga wake.

“Hivi vyama bado ni vichanga, havina capacity (uwezo) kama ilivyo CCM. Kweli kuna changamoto nyingi, leo kuna changamoto hii, kesho kuna hii, lakini kubwa ni kuwahusisha wananchi, tupate nafasi ya kuzungumza na wanachama, kujadiliana nao na kufanya nao kazi kutatua changamoto zilizopo,” alisema Lowassa ambaye alikuwa Waziri Mkuu kuanzia mwaka 2005 hadi 2008 alipojiuzulu.

Kuhusu Chadema, alisema chama hicho kikuu cha upinzani kinakua haraka, kinaongeza idadi ya wanachama na viongozi wengi, hivyo akasema kinachotakiwa ni kujenga uwezo wao.

Alisema uzoefu huo hauwezi kuja kwa siku moja, bali kwa muda mrefu kama ilivyo kwa CCM.

“CCM ni moja ya vyama vikongwe Afrika na ina uzoefu mkubwa. Ukitulinganisha sisi (utaona) tuko nyuma yao, lakini tunayo majukumu makubwa na makali zaidi mbele yetu kuliko wao,” alisema.

Mwanasiasa hiyo alisema Watanzania wanajua, wanaona na wanasikia kwamba vyama vya upinzani vinanyimwa haki hiyo.

“Pamoja na kura milioni sita tulizozipata za urais, hatuna haki. Haturuhusiwi kufanya mikutano ya hadhara. Hili ni jambo gumu sana kulielewa. Ni jambo baya sana katika demokrasia,” alisema.

“Ni jambo lisilokubalika katika jamii ya kimataifa, lakini imewekwa kwamba ukifanya mkutano wa hadhara unakamatwa unapelekwa mahakamani.

“Sasa hiyo inatunyima nafasi ya kuwasiliana na wanachama wetu. Lakini Katiba ya nchi hii imeruhusu vyama vya siasa vishindane bila kupigana. Tupingane bila kupigana. Vyama vimeruhusiwa kufanya hivyo. Serikali kuzuia mikutano ya hadhara ni blow (pigo) kubwa kuliko zote tulizopata katika uongozi wa vyama vya upinzani.”

Alisema kuzuia mikutano ni kuwakwaza wananchi.

“Kama hatupati nafasi ya kushindanisha sera zenu, mtakuwa mnawakwaza wananchi na mtakuwa mnakwaza demokrasia katika nchi,” alisema.

Licha ya kauli hizo, ilipofika Machi 1, 2019, alienda katika Ofisi Ndogo za CCM zilizopo Mtaa wa Lumumba jijini Dar es Salaam na kupokewa na viongozi wa juu wa CCM, huku yeye akisema ameamua kurudi nyumbani (CCM).

"Nimetafakari na sasa nimeamua kurudi nyumbani CCM ambako sehemu kubwa ya maisha yangu nimekuwa huko," alisema Lowassa.

Lowassa alichomoka CCM Julai 27, 2015 ikiwa ni siku chache baada ya Kamati Kuu ya CCM kuondoa jina lake na mengine katika kinyang’anyiro cha urais, uamuzi ambao ulizua mtafaruku uliosababisha wajumbe wa Halmashauri Kuu kuimba wimbo wa kuonyesha kuwa na imani naye wakati mwenyekiti wa wakati huo, Jakaya Kikwete akiingia mkutanoni.

Siku moja baada ya kujiengua CCM, Lowassa alitangaza kujiunga na Chadema, chama ambacho kilimpa fursa ya kuendeleza “Safari ya Matumaini”, kwa kushirikiana na vyama vingine vitatu vilivyoundwa Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa).

Chanzo: Mwananchi
Related Articles: