Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Julius Kalanga: Haikuwa rahisi kuvaa viatu vya Lowassa, Monduli

Julius Kalanga Aliyekuwa mbunge wa Monduli, Julius Kalanga

Sat, 10 Feb 2024 Chanzo: Mwananchi

Aliyekuwa mbunge wa Monduli, Julius Kalanga amezungumzia kifo cha Waziri Mkuu wa zamani, Edward Lowassa akikiri ugumu wa kupokea kijiti cha ubunge kutoka kwake kutokana na rekodi aliyokuwa ameiweka katika jimbo hilo.

Lowassa amefariki leo Februari 10, 2024 kutokana na maradhi ya kujikunja kwa utumbo, mapafu na shinikizo la damu, kwa mujibu wa Makamu wa Rais, Dk Philip Mpango ambaye ametangaza kifo chake.

Akizungumzia kifo cha Lowassa leo Februari 10, 2024, Kalanga ambaye kwa sasa ni Mkuu wa Wilaya ya Karagwe, mkoani Kagera, amesema akiwa kama kijana wakati alipopata nafasi ya kushika wadhifa wa ubunge baada ya Lowasa kuamua kutogombea tena nafasi hiyo, anakiri ugumu alioupata kuvaa viatu vya mtangulizi wake ambaye amefanya mambo makubwa ya kimaendeleo katika jimbo la Monduli na Taifa kwa ujumla.

Kalanga ambaye alikuwa mbunge wa jimbo hilo kuanzia mwaka 2015 hadi 2020, amesema msiba huu ni mkubwa kwa Taifa ila kwa Monduli wamempoteza baba na mlezi ambaye alilibadilisha eneo hilo.

Ametaja baadhi ya mambo makubwa aliyoyafanya Lowassa kuwa ni pamoja na kuasisi uanzishwaji wa shule za kata katika ngazi ya Taifa pamoja na eneo lake la Monduli ambalo lilionekana kuwa na mwamko mdogo wa elimu.

Amesema jitihada za Lowassa zimefanya wilaya hiyo kuwa miongoni mwa maeneo ya jamii za wafugaji yenye mwamko mkubwa wa elimu, pamoja na shule za msingi na sekondari zikiwemo za bweni.

“Kwanza nilijiona kijana mwenye bahati ya kupokea madaraka kwa kiongozi mkubwa mahiri mwenye heshima na aliyetukuka kwa utumishi wake. Nilijiona napokea mzigo ambao kwa kweli viatu vyake vilikuwa vikubwa na vingekuwa vikubwa kwa mtu yoyote yule aliyekuwa akiingia kwa mzee Lowassa, niliona ni heshima kubwa na bahati kupokea kijiti kutoka kwake.”

“Nakumbuka Lowassa ni kama alinirithisha jimbo kwa maana siyo jimbo la kugombea ni kwamba aliacha kwa hiari yake, akanishika mkono, nikawa mbunge wa Monduli, kwa hiyo ameweka historia katika maisha na familia yangu na najiona mwenye bahati kupokea kutoka kwake,” ameongeza.

Chanzo: Mwananchi
Related Articles: