Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

CCM yamlilia Lowassa

Makonda X Lowassa CCM yamlilia Lowassa

Sat, 10 Feb 2024 Chanzo: Mwananchi

Chama cha Mapinduzi (CCM) kimehuzunishwa na kifo cha Waziri Mkuu mstaafu, Edward Lowassa kikisema mwanasiasa huyo atakumbukwa kwa umahiri wake wa kujenga hoja katika nyakati tofauti na kufanya kazi kwa bidii.

Katibu wa Itikadi, Uenezi na Mafunzo wa CCM, Paul Makonda amesema CCM inaungana na mwenyekiti wake, Rais Samia Suluhu Hassan kutoa pole kwa familia ya Lowassa na kumwomba Mungu awape uvumilivu katika kipindi hiki kigumu cha msiba.

Lowassa aliyehudumu katika nafasi ya uwaziri mkuu kwa miaka mitatu kati ya mwaka 2005 hadi 2008 katika Serikali ya awamu ya nne iliyoongozwa na Rais mstaafu, Jakaya Kikwete, amefariki dunia leo Februari 10, 2024 wakati akipatiwa matibabu katika Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete (JKCI) baada ya kuugua kwa muda mrefu.

“Kwa niaba ya Chama cha Mapinduzi (CCM) tunatoa pole kwa wanachama, wapenzi wakeretwa wa CCM na Watanzania, kwa kuwa alikuwa kiongozi mwema na ametoa mchango wa Taifa katika nafasi alizozitumikia.”

“Hatuna budi kukubaliana na kazi ya Mungu, najaribu kupanga maneno yananishinda kwa sababu wakati naanza ziara hii, Dar es Salaam nikaenda Pwani, Tanga, Kilimanjaro na Arusha nilifika jimbo la Monduli linalongozwa na Fredrick Lowassa,” amesema Makonda katika mkutano wa hadhara uliofanyika uwanja wa shule ya msingi Matarawe wilayani Songea mkoani Ruvuma.

Makonda amesema katika ziara yake alipofika Monduli, jimbo la zamani la Lowassa na alimkumbuka mwanasiasa huyo katika utumishi wake wa Serikali, lakini hakujua kwamba kabla ya kuhitimisha ziara yake atapata taarifa nzito ya kifo chake.

“Yote ni mapenzi ya Mungu, Rais (Samia Suluhu) ameshatangaza maombelezo na kushusha bendera kwa siku tano, kupitia tangazo hilo sisi kama chama tunajipanga kusubiri utaratibu ili tuweze kushiriki katika mazishi,” amesema Makonda.

Chanzo: Mwananchi
Related Articles: