MUIGIZAJI maarufu wa Filamu nchini Marekani na duniani kwa ujumla Will Smith ametangaza kujiuzulu katika Tuzo za Oscar na yupo tayari kwa adhabu nyingine ya ziada.
Katika taarifa iliyotolewa na Smith amesema kitendo cha kumpiga kofi Mchekeshaji Chris Rock ukumbini ni kitendo cha kushitusha, kinaumiza na hakistahili kusameheka na akaongeza kwa kusema yupo tayari kukubali adhabu nyingine yoyote itakayotolewa na Bodi ya Waandaaji wa Tuzo za Oscar.
Smith kwenye taarifa yake alisema: “Idadi ya watu niliowaumiza kutokana na tukio lile ni Chris, familia yake, rafiki zangu wapendwa na mashabiki wote duniani, Nimeharibu imani ya ya Taasisi hii na nimeharibu heshima ya washindi wa mwanzo wa tuzo hizi ambao nawanyima nafasi ya kuifurahia na kufurahiwa.”
Waandaaji wa Tuzo ya Oscar wamenukuliwa kukubali kupokea barua ya kujiuzulu ya Will Smith na kudai kuwa wataendelea na hatua nyingine za uchunguzi na hatimaye watatoa taarifa rasmi ya kile kitakachoamuliwa juu ya Will Smith.
Watu wa karibu wa Taasisi hiyo wanaamini hatua itakayochukuliwa itakuwa ni Will Smith kunyang’anywa tuzo hiyo ambayo ndiyo aliipata kwa mara ya kwanza katika historia ya maisha yake.
Watu wa karibu na Smith wanaamini kuwa hata hatima ya kazi zake nyingine zinazofuata zinazodhaminiwa na Kampuni ya Apple hasa zile za Slave Escape pamoja na zile za uchekeshaji zote zitasimama.
Katika tukio hilo la kumpiga kofi mchekeshaji huyo Askari kutoka Idara ya Polisi ya Jiji la Los Angels walitaka kumkamata kwa nguvu Will Smith na kumuondoa ukumbini lakini katika hali ya kushangaza Chris Rock alionesha kutokukubaliana na mpango huo na kuwataka wamuache Smith aondoke mwenyewe bila matumizi ya nguvu.
Aprili 18 ndiyo tarehe ambayo Will Smith anatarajiwa kujua endapo ataendelea kuwa na Tuzo hiyo na zaidi kabisa ni kujua hatima ya kazi yake.
Chris Rock ambaye alionekana kwenye shoo yake Boston hadi sasa hajatoa tamko lolote kuhusiana na tukio lile, alipohojiwa wakati wa shoo yake aliahidi kuwa atatoa tamko pale utakapofika muda muafaka.