Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Kocha Nabi aivuruga Bandari FC

IMG 20230621 WA0146 Kocha Nabi na Twaha

Wed, 21 Jun 2023 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Picha zilizozagaa mitandaoni zikimuonyesha Naibu Mwenyekiti wa Bodi ya Bandari FC, Twaha Mbarak, akiwa na aliyekuwa kocha mkuu wa Yanga ya Tanzania, Nasreddine Nabi, zimezua tetesi huenda ndiye anachukua mikoba ya Anthony ‘Modo’ Kimani.

Nabi amejitengenezea heshima Bongo akiiongoza Yanga kufika fainali ya Kombe la Shirikisho Afrika na pia kutetea ubingwa wa Ligi Kuu Tanzania Bara na Kombe la FA nchini humo maarufu Azam Sports Federation Cup.

Hata hivyo Twaha ambaye alikua jijini Dar es Salaam kushuhudia mechi ya kufuzu Kombe la Afrika 2023 kati ya wenyeji Tanzania dhidi ya Niger, alikanusha uvumi wa kocha Nabbi kutua Bandari FC.

Akizungumza nasi kwa njia ya simu kutoka Bongo, Twaha alisema kocha huyo raia wa Tunisia anaelekea nchini Afrika Kusini kujiunga na vigogo Kaizer Chiefs huku akisisitiza Nabbi sio miongoni mwa makocha kwenye rada zao.

“Nabi mwenyewe amenidhibitishia anakwenda Afrika Kusini kuwa mkufunzi wa Kaizer Chiefs, hayupo kwenye listi ya makocha tunaofanya mazungumzo nao,” alisema Twaha.

Lakini taarifa kutoka Afrika Kusini zinasema mazungumzo kati ya kocha Nabi na klabu ya Kaizer Chiefs yamesimama kutokana na uongozi wa klabu hiyo kugawanyika kuachana au kuendelea na kocha wao Arthur Zwane.

Twaha alisema wanatarajia kumtangaza kocha mpya wa Bandari FC baada ya gemu ya mwisho wa msimu huu dhidi ya Posta Rangers itakayopigwa Jumapili jijini Nairobi.

Miongoni mwa makocha wanaohisishwa na Bandari FC ambayo kwasasa ipo chini ya kaimu kocha Twahir Muhiddin ni Patrick Aussems wa AFC Leopards, Salim Babu wa Nzoia Sugar, Robert Matano wa Tusker FC na aliyewahi kuwa kocha wa Harambee Stars, Francis Kimanzi.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live
Related Articles: