Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Mbowe, Lissu wakinukisha operesheni ‘+255Katiba Mpya Okoa Bandari zetu’

Picha Mbowe Data Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe akihutubia mkutano wa hadhara mjini Bukoba.

Sat, 29 Jul 2023 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Wamekiwasha! Ndivyo inavyoweza kusemwa kwa lugha na semi zilizozoeleka mitaani kuzungumzia uzinduzi wa mikutano ya hadhara ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) kupitia operesheni ‘+255 Katiba Mpya Okoa Bandari zetu’

Hii ni baada ya viongozi wakuu wa Chadema wakiongozwa na Mwenyekiti wao, Freeman Mbowe kuushambulia jukwaa kwa hoja tofauti likiwemo suala la mkataba wa uwekezaji bandarini, Katiba Mpya, matumizi ya rasilimali za Taifa na hali ngumu ya kiuchumi kwa wananchi mijini na vijijini.

Akihutubia mkutano huo leo Julai 28, 2023 katika uwanja wa Uhuru maarufu kama uwanja wa Mayunga mjini Bukoba, Mbowe amesema kutokana na rasilimali zilizopo nchini na muda wa miaka zaidi ya 60 ya Uhuru, Tanzania inastahili kuwa miongoni mwa Mataifa ya Afrika yenye uchumi imara na maendeleo ya watu na vitu; lakini hali ni tofauti kutokana na kile anachodai ni kukosekana kwa uongozi bora.

‘’Mkoa wa Kagera ni miongoni mwa mikoa nchini iliyojaaliwa ardhi nzuri yenye, hali nzuri ya hewa, watu zaidi ya milioni mbili, mazingira na fursa nzuri ya kibiashara; lakini watu wake wanaishi katika hali ngumu. Wenye dhamana ya uongozi wamshindwa na wanastahili kuondoka madarakani,’’ amesema Mbowe

Uwekezaji bandarini

Akizungumzia mjadala uliopamba moto nchini kuhusu mkataba kati ya Serikali ya Tanzania na Dubai kuhusu uwekezaji bandarini, Mbowe amewasihi Watanzania kujadili na kutoa maoni yao kwa uhuru bila kujali tofauti zao kiimani, kisiasa wala maeneo yao ya Kijiografia kwa sababu suala hilo linahusu maslahi ya Taifa kuanzia vizazi vya sasa na vijavyo.

"Kwenye suala la mkataba wa bandari hakuna udini, itikadi wala maeneo tunayotoka. Kamwe tusikubali kugawanyika katika hili,’’ amesema Mbowe

Akizungumzia mkataba huo, Makamu Mwenyekiti wa Chadema, Tundu Lissu (Bara) amewasihi Watanzania kujitokeza kwa uwazi na ujasiri kuiohoji Serikali kuhusu maslahi na faida ya Taifa katika uwekezaji huo.

Amesema tofauti na mikataba kadhaa ya uwekezaji na ubinafsisha iliyowahi kuingiwa na Serikali, mkataba wa uwekezaji bandarini umeibua jambo jipya ambalo halijawahi kushuhudiwa la viongozi wakuu wa Chama Cha Mapindizi (CCM) na watendaji serikalini kujitokeza na wengine kuzunguka maeneo mbalimbali nchini kushawishi umma.

“Tumeingia mikataba mingi ya kubinafasisha mashirika na taasisi za umma tangu wakati wa uongozi wa Benjamin Mkapa, Jakaya Kikwete na John Magufuli, hatujaona viongozi wakizunguka kushawishi umma kuwa mkataba uko sawa. Watanzania tusioope kuhoji na kukosoa; na ni wajibu wa Serikali kujibu hoja badala ya kudhibiti ukosoaji,’’ amesema Lissu

Amesema ukosoaji huo unapaswa kufanyika bila kuingiza masuala ya kiitikadi, imani za kidini wala maeneo ya Kijiografia huku akiwaonya wanaojaribu kuingiza udini, itikadi na taofauti ya maeneo kati ya wakosoaji na wanaounga mkono mkataba wa uwekezaji bandarini.

‘’Nimekosoa, kuonya na kushauri tangu enzi za Benjamin Mkapa, Jakaya Kikwete na John Magufuli; tena Mzee Mkapa na Magufuli naambiwa walikuwa waumini wa Kanisa Katoliki kama mimi na niliwakosoa kwa matendo na makosa yao. Nawashangaa wanaoingiza udini katika suala uwekezaji bandarini,’’ amesema Lissu

Katiba Mpya

Akihutubia mkutano huo, Katibu Mkuu wa Chadema, John Mnyika amesisitiza msimamo wa chama hicho kikuu cha upinzani kuhusu Katiba Mpya kabla ya chaguzi zijazo kuanzia ule wa Serikali za Mitaa mwaka 2024 na uchaguzi mkuu wa mwaka 2025.

‘’Ofisi ya Waziri Mkuu imeviandikia vyama vya siasa na asasi za kiraia kutaka maoni kuwezesha kuandika upya sheria ya uchaguzi na vyama vya siasa. Hii ni ishara ya kujiandaa kuingia kwenye uchaguzi wa Serikali za mitaa mwaka 2024 na uchaguzi mkuu mwaka 2025 bila Katiba Mpya….tatizo la Watanzania siyo sheria ya uchaguzi wala vyama vya siasa, bali ni Katiba,’’ amesema Mnyika

Ametaja miongoni mwa kasoro za Katiba ya sasa kuwa ni kumpa Rais ambaye pia ni Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) mamlaka ya kuwateua viongozi na watendaji wa Tume ya Uchaguzi akiwemo Mwenyekiti, wajumbe na wale wa halmashauri; jambo linalofanya uwanja wa siasa kutokuwa sawa kwa washindani wote.

‘’Tunachotaka ni Katiba Mpya au mabadiliko makubwa ya Katiba kuondoa kasoro zote zinazofanya chaguzi zetu kutokuwa huru,’’ amesema Mtendaji mkuu huyo wa Chadema

Mnyika amesema madai ya Katiba Mpya bora inapaswa kuwa ajenda ya Watanzania wote bila kujali itikadi, imani zao kidini wala maeneo yao ya Kijiografia kwa sababu hasara ya Katiba mbaya inawakumba wote kama ilivyo pia faida na manufaa ya Katiba bora.

Hoja ya Katiba Mpya imeungwa mkono na Makamu Mwenyekiti wa Chadema, Tundu Lissu (Bara) akisema Taifa linahitaji Katiba ambayo siyo tu itawadhibiti na kuwawajibisha viongozi, bali pia kulinda mali na rasilimali za Taifa kwa faida na maslahi ya umma.

Mbunge huyo wa zamani wa Singida Mashariki amesema Taifa linahitaji Katiba ambayo siyo tu itaweka misingi ya kuwadhibiti viongozi walioko madarakani bila kujali itikadi zao kisiasa, bali pia inayotoa fursa kwa umma, mamlaka na taasisi huru kuwawajibisha viongozi kwa makosa yao tofauti na sasa ambapo wamejiwekea kinga ya kutoshtakiwa.

Chaguzi zijazo

Kuhusu chaguzi zijazo mwaka 2024 na 2025, Katibu Mkuu wa Chadema, John Mnyika amewataka wana Chadema wenye nia ya kugombea nafasi mbalimbali za uongozi kwa tiketi ya chama hicho kujitokeza kutangaza nia na kushiriki ujenzi wa chama tayari kwa ushinda kupitia sanduku la kura na kushika dola.

‘’Kupitia kampeni yetu ya ‘+255Katiba Mpya Okoa Bandari zetu’ Chadema tutawasajili wanachama na kuwapa kadi mpya za kidijitali kwa lengo la kujiimarisha, kurahisisha na kuboresha mawasiliano ya moja kwa moja na wanachama kwa njia ya kidijitali ikiwemo ujumbe mfupi wa maneno,’’ amesema Mnyika

Muungano

Naibu Katibu Mkuu wa Chadema, Salum Mwalim (Zanzibar) amewataka Watanzania kuulinda Muungano huku wakipigania suala la mabadiliko ya kimuundo kwa sababu una manufaa nyingi kijamii na kwa Taifa.

‘’Mimi nitakuwa mtu wa mwisho kupiga kura kuuvunja Muungano kwa sababu una faida nyingi. Lakini pia nitakuwa wa kwanza kupiga kura kudai marekebisho ya muundo wa Muungano wetu kuwa wa Serikali kamili ya Tanganyika na Zanzibar kuondoa kasoro, kero na malalamiko kutoka pande zote ikiwemo lile la Wazanzibari kuhisi Tanganyika imevaa koti la Muungano,’’ amesema Mwalimu

Akifafanua, Mwalim ambaye ni mwandishi wa habari kitaaluma amesema kitendo cha baadhi ya Mawaziri wa Wizara za Muungano kuiwakilisha Zanzibar katika mambo yasiyo ya Muungano ikiwemo elimu na afya ni miongoni mwa hoja zinazwafanya Wazanzibari kuhisi kuwa Tanganyika imevaa koti la Muungano. Imeandikwa na Saada Amir, Mgongo Kaitira na Damian Masyenene.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live
Related Articles: