Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Uamuzi kesi ya mkataba wa bandari Agosti 7

Kesi 33 Bandari Wakili Mwabukusi

Sat, 29 Jul 2023 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Hatima ya uhalali wa mkataba wa makubaliano ya ushirikiano wa kiuchumi na kijamii, kati ya Serikali ya Tanzania na Dubai (IGA), utajulikana Agosti 7, mwaka huu, pale Mahakama Kuu Kanda ya Mbeya itakapotoa uamuzi wa kesi ya kupinga makubaliano hayo.

Mahakama imepanga kutoa uamuzi wake tarehe hiyo, leo Julai 28, 2023, baada ya kukamilisha usikilizwaji wa hoja za pande zote katika kesi hiyo.

Usikilizwaji wa kesi hiyo umehitimishwa jana na mawakili wa upande wa walalamikaji, ambao wamefunga pazia la usikilizwaji wa kesi hiyo kwa kuwasilisha hoja za ziada kujibu hoja za mawakili wa Serikali.

"Baada ya kutamka hayo, niseme kwamba Mahakama itatoa uamuzi Agosti 7, 2023 Jumatatu saa 3:00 asubuhi," amesema Jaji Dunstan Ndunguru, Kiongozi wa jopo la majaji watatu walioisikiliza kesi hiyo.

Kabla ya kutaja tarehe hiyo na kisha kuahirisha kesi hiyo, Jaji Ndunguru amewapongeza mawakili wa pande zote kwa hoja zao walizowasilisha pamoja na wananchi waliokuwa wakiifuatilia kesi hiyo mahakamani hapo, kwa niaba ya majaji wenzake, Mustafa Ismail na Abdi Kagomba.

Kesi hiyo ya kikatiba namba 5 ya mwaka 2023 imefunguliwa na Watanzania wanne kutoka mikoa tofauti tofauti ambao ni Alphonce Lusako, Emmanuel Chengula, Raphael Ngonde na Frank Nyalus dhidi ya Serikali.

Wadaiwa ni Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG), ambaye ni mshauri wa Serikali kwa mausuala ya kisheria, Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, Katibu Mkuu Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi na Katibu wa Bunge la Tanzania, ambaye ni mtendaji mkuu na mratibu wa shughuli za Bunge.

Katika kesi hiyo wanapinga makubaliano hayo yanayohusisha uwekezaji katika bandari za Tanzania zilizoko katika mwambao wa bahari na katika maziwa, kuwa ni batili kwa kuwa yana ibara zinazokiuka Sheria na Katiba ya Nchi.

Pia wanadai kuwa mchakato wa kuridhia bungeni ni batili kwa kuwa haukufuata utaratibu wa kisheria na bila kuwapa nafasi ya kutosha wananchi kutoa maoni yao kama sheria za nchi zinavyoelekeza.

Kesi hiyo ilianza kusikilizwa rasmi Jumatano Julai 26, siku moja baada ya mawakili wa pande zote kuandaa na kuwasilisha mahakamani hoja za msingi walizokubaliana kuwa ndizo zinazobishaniwa, yaani viini vya kesi ambavyo ndivyo Mahakama itavizingatia katika kutoa uamuzi wake.

Mawakili wote walikubaliana na kuwasilisha jumla ya hoja mano kabla ya Mahakama yenyewe kuongeza moja na hivyo kuwa hoja sita.

Baada ya kukamilika kwa hoja hizo, mawakili wa walalamikaji ambao ni Mpale Mpoki, Boniface Mwabukusi, Livino Ngalimitumba na Philipo Mwakilima, walianza kuwasilisha hoja zao.

Katika mawasilisho yao ya hoja mawakili hao walichambua ibara zote za mkataba huo wanazozipinga na kuonesha kile wanachodai kuwa ni masharti mabovu yasiyo na maslahi kwa Taifa na jinsi unavyokiuka sheria na Katiba ya nchi.

Walifafanua madai yao ili kuishawishi mahakama kuwa mkataba huo ni batili kwa kuwa na ibara hizi zina masharti yanayokiuka Sheria za Ulinzi wa Raslimali na Maliasili za Nchi, Katiba na kwamba unaondoa ukuu wa Nchi na kuiweka chini ya Dubai na vile vile kuathiri Maliasili za Taifa na kuhatarisha usalama wa Taifa.

Pia walifafanua madai yao ya mchakato wa kuridhiwa na Bunge ulivyoikuka Sheria kwa kutowapa wananchi kwanza nafasi ya kutoa maoni yao kabla ya kuridhiwa kama sheria zinavyoelekeza.

Vilevile walifafanua madai yao kuwa ni batili kutokana kwa madai kwamba Dubai haina mamlaka kuingia mkataba wa kimataifa kama huu kwa mujibu wa Ibara ya 123 ya Katiba ya Umoja wa Falme za Kiarabu (UAE) na kwamba jukumu hilo linapaswa kufanywa na Serikali ya Umoja huo.

Baada ya kumaliza hoja zao, jopo la mawakili wa Serikali linaloongozwa na Wakili wa Serikali Mkuu, Mark Mlwambo nao walianza kujibu hoja za mawakili wa utetezi na kuhitimisha jukumu hilo jana Alhamis Julai 27, 2023.

Katika kujibu hoja hizo mawakili hao wa Serikali, Wakili Mkuu wa Serikali Edson Mweyungee na mawakili wa Serikali Stanley Kalokola na Edwin Webiro kwa nyakati tofauti nao walichambua ibara mbalimbali za mkataba huo zinazolalamikiwa, wakilinganisha na vifungu vya sheria za nchi na ibara za Katiba ya nchi .

Hata hivyo baada ya kufanya uchambuzi huo walihitimisha kwa kudai kuwa hakuna kifungu chochote cha Sheria wala ibara ya Katiba iliyokiukwa.

Katika ujumla wake wamedai kuwa mkataba huo unaolalamikiwa ni mkataba wa kimataifa hivyo utekelezaji wake hauongozwi na sheria za nchi bali sheria za kimataifa kama Mkataba wa Kimataifa wa Vienna unavyoeleza kuhusu utekelezaji wa mikataba ya kimataifa, ambao Tanzania imeusaini na kuwa mwanachama.

Akihitimisha hoja hizo Wakili Mlwamba aliiomba Mahakama kulitupilia mbali kesi hiyo na kuiomba iwaamuri wadai wailipe Serikali gharama za kesi hiyo. Baada ya mawakili wa Serikali kuhitimisha hoja zao mawakili wa walalamikaji walipata nafasi nyingine kujibu hoja zilizoibuliwa na mawakili wa Serikali wakati walijibu hoja zao kuanzia jana na kuhitimisha leo.

Baada ya kuchambua majibu ya mawakili wa Serikali mawakili hao wa walalamikaji wamehitimisha hoja zao, wakisisitiza kuwa wameweza kujibu madai yao na kwamba wadaiwa (mawakili) katika hoja zao wameshindwa kuyakanusha.

Nje ya mahakama baada ya kesi kuahirishwa wakili Mwabukusi amewaeleza wanahabari na wananchi waliojitokeza kufuatilia kesi hiyo kuwa wamefanya kwa akili uwezo na ujuzi wao wote kile kwa walichopaswa kukifanya katika kesi hiyo mahakamani, na kwamba sasa anakwenda majukwaani kupambana kisiasa.

Amesema kuwa baada ya kumaliza kesi anakwenda kukung'uta joho la uwakili na anakwenda majukwaani kupambana na wanasiasa wanaizunguka nchini katika majukwaa ya kisiasa kuutetea mkataba huo na kwamba mpaka mwenye kampuni ya Dubai Ports World (DP World) iliyopewa uwekezaji bandarini ajitokeze.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live
Related Articles: