Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Serikali yajibu hoja sakata la bandari

Wabunge EALA Wahadharisha Ubaguzi Uwekezaji Wa Bandari Wakati hoja mbalimbali zikiendelea kutolewa kuhusu mkataba wa uendelezaji na uboreshaji wa bandari b

Thu, 22 Jun 2023 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Wakati hoja mbalimbali zikiendelea kutolewa kuhusu mkataba wa uendelezaji na uboreshaji wa bandari baina ya Tanzania na Dubai, Serikali imesema haitoi uhuru wake kwa kampuni ya DP World inayokwenda kutekeleza mkataba huo.

Maelezo hayo ya Serikali yanalenga kujibu wachambuzi wanaokosoa kipengele cha 4 cha mkataba huo kinachosema; “Tanzania itakuwa na haki ya kuitaarifu Serikali ya Dubai kuhusu fursa nyingine za uwekezaji katika maeneo ya bandari na maeneo huru, ili kuwezesha taasisi za Dubai kuwasilisha mapendekezo ya uwekezaji katika maeneo hayo.

“DPW na washirika wake ndio watakuwa na jukumu la kutafuta fedha za uwekezaji kwa ajili ya uwekezaji na Tanzania kama itakuwa na maeneo mengine ya uendelezaji wa bandari, inabidi kampuni ya DP World ipewe taarifa kwanza.”

Kifungu hiki kimekuwa kinaelezwa na wanasheria na wadau mbalimbali, akiwemo aliyewahi kuwa Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Profesa Anna Tibaijuka, kuwa kinaingilia uhuru wa nchi kujiamulia mambo yake.

Hivyo, Profesa Tibaijuka na wadau wengine wameshauri hilo liwe miongoni mwa maeneo ya kufanyiwa marekebisho, la sivyo mkataba huo unahatarisha ulinzi na usalama wa nchi.

Kufuatia mjadala huo, jana watendaji kadhaa wa Serikali wakiongozwa na Naibu Katibu Mkuu Uchukuzi, Dk Ally Possi walitolea ufafanuzi baadhi ya hoja zinazoibuliwa walipozungumza katika kipinci cha Power Breakfast cha Redio Clouds.

Kuhusu hoja ya uhuru wa nchi, Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania (TPA), Plasduce Mbossa alisema “kwa hali ya kawaida haiwezekani Tanzania kutoa uhuru wake kwa kampuni ya DP World.”

Kuhusu nguvu ya Tanzania endapo kampuni hiyo itawekeza kwa washindani na kudhoofisha bandari za Tanzania, Mbossa alisema kwenye mkataba wa makubaliano kutakuwa na mikataba midogo midogo itakayokuwa na vipengele ambavyo DP World itapaswa kutekeleza na endapo itavikiuka itakuwa imevunja mkataba mzima.

“Kwa kawaida, tunapoingia mikataba ya uwekezaji kuna masharti tunawekeana, kuna vitu wanatwambia tusivifanye na wao tunawaambia wasivifanye; haiwezekani tukakupa bandari yetu ukaenda kuungana na bandari shindani, kwetu sisi inaweza kuwa kigezo cha kusitisha mkataba.

“Lakini anaweza akawa anafanya eneo lingine tukaona sisi anaweza kutusaidia kupata mzigo kutoka hiyo sehemu, mfano akiwa Maputo Msumbiji, badala ya kuutoa mzigo Congo kuupeleka Maputo, atautoa Congo kuuleta Dar es Salaam,” alisema.

Ulinzi wa nchi

Kuhusu mkataba huo kuhatarisha ulinzi na usalama wa Tanzania, Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Anga Tanzania (TCAA), Hamza Johari alisema suala la ulinzi na usalama wa nchi halipaswi kutiliwa shaka.

Alisema kampuni binafsi ya kimataifa ya kuhudumia makontena Tanzania (TICTS), imefanya kazi bandarini kwa miaka 20 na suala la ulinzi na usalama halijawahi kuwa changamoto kwa kuwa lipo chini ya Serikali.

“TPA na vyombo vya ulinzi na usalama vinafanya jukumu hilo, kabla ya chombo kuingia nchini, kinakaguliwa hukohuko, ndipo kinaruhusiwa kuingia nchini,” alisema.

Dubai haionekani?

Akijibu hoja ya baadhi ya wadau kwa nini Serikali imeingia makubaliano na kampuni badala ya Serikali ya Dubai, Dk Possi alisema kwenye mkataba huo Serikali ni shahidi namba moja.

“Ibara ya 31, 28 na 25 ya mkataba inasema, baada ya nchi zote kuridhia mkataba huo, kila nchi zitabadilishana nyaraka ya uthibitisho kuwa kila nchi imeridhia.

Alisema kwenye mkataba huo, Dubai ni shahidi namba moja kwa sababu imekasimiwa madaraka na nchi za Falme za Kiarabu katika masuala ya uwekezaji.

Akijibu hoja ya kwa nini mkataba unagusa eneo la maziwa, Dk Possi alisema lengo ni kuongeza ufanisi.

Alisema uwekezaji utakaofanyika kwenye Bandari ya Dar es Salaam ili uwe na tija, lazima eneo la maziwa nako kufanyiwe maboresho.

“Miradi ya kimkakati ambayo Serikali inaitekeleza, lengo ni kuendeleza sekta ya uchukuzi. Reli haitakuwa na maana kama meli tunazojenga kwa ajili ya kubeba mizigo kutoka Bandari ya Dar es Salaam kufika DRC na Uganda hazitatumika kuisafirisha.

“Tumejenga reli ya kisasa ambayo itafika Kigoma, mtu amepakia mzigo anafika Bandari ya Kigoma ule ufanisi unakuwa hauna maana (kama ziwa halitatumika),” alisema.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live
Related Articles: