Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Prof Mkumbo: DP World haikupendelewa uwekezaji bandarini

Kitila Mkumbo Prof Mkumbo.

Mon, 31 Jul 2023 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Waziri wa Mipango na Uwekezaji, Profesa Kitila Mkumbo amesema kampuni ya DP World kutoka Dubai haikupendelea kupewa fursa ya kuwekeza katika Bandari ya Dar es Salaam kupitia mkataba wa makubaliano ya uwekezaji kati ya Serikali ya Tanzania na Dubai.

Akizungumza jijini Mwanza jana Julai 30, 2023 wakati wa mkutano wa hadhara wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Profesa Mkumbo amesema kampuni hiyo imepata fursa hiyo baada ya uchambuzi wa kina wa jopo la wataalam wa Serikali kupitia mapendekezo ya makampuni saba ya nje yaliyojitokeza kuomba kuwekeza katika bandari ya Dar es Salaam.

Profesa Kitila amesema pamoja na mambo mengine, mapendekezo ya kampuni ya DP World yenye uzoefu wa kuwekeza katika bandari za nchi takriban 60 yalibainika kuwa bora na yenye manufaa zaidi kwa Taifa ndio maana ikapata fursa hiyo.

"Kampuni saba zikiwamo za India, Falme za Kiarabu, China na Ulaya zilishindanishwa kupata fursa ya kuwekeza bandarini; na baada ya uchambuzi, kampuni ya DP World ikapendekezwa. Hivyo siyo kweli kwamba hakukuwa na kampuni zilizoshindanishwa," amesema Mkumbo

Huku akishangiliwa na umati wa wananchi waliohudhuria mkutano huo wa Katibu Mkuu wa CCM, Daniel Chongolo, Profesa Mkumbo ametetea uamuzi wa Bunge wa kupitisha mkataba wa uwekezaji kati ya Serikali ya Tanzania na Dubai akisema una manufaa na maslahi kwa Taifa.

Amesema licha ya kuongeza tija badnarini, utekelezaji wa mkataba huo pia utawaongezea utaalam na kulinda ajira za Watanzania walioajiriwa bandarini.

"Kuwa na rasilimali pekee hakutoshi, lazima tuwekeze na kuchangamkia fursa za kiuchumi nchini; tuongeza mapato ya Serikali na uwezo wa kugharamia utekelezaji wa miradi ya maendeleo,’’ amesema

Bila kufafanua, Waziri huyo ameahidi kuwa Serikali na Bunge itazingatia maoni ya Watanzania kuhusu mikataba ya uwekezaji kwa faida na maslahi ya umma na Taifa kwa ujumla.

Mwenyekiti wa Kamati ya kudumu ya Bunge ya Uwekezaji wa Mitaji ya Serikali, Jerry Silaa amesema CCM na Serikali inalazimika kufanya mikutano katika maeneo mbalimbali nchini kutoa ufafanuzi kuhusu mkataba wa uwekezaji bandarini kujibu maswali na kutoa ufafanuzi wa hoja mbalimbali zinazoibuliwa kuhusu mkataba huo.

"Ndugu zangu wa Kanda ya Ziwa na Watanzani wote nawahakikishia kwamba ushauri na maoni inayotolewa kwa nia njema itafanyiwa kazi wakati wa kuingia kwenye mikataba ya uwekezaji,’’ amesema Silaa

Waziri wa Mipango na Uwekezaji, Profesa Kitila Mkumbo naye amesisitiza ahadi ya Serikali kusikiliza, kuchukua na kuzingatia hoja na ushauri wenye nia ya kuboresha mkataba na kuongeza tija kwenye uwekezaji bandarini.

Hata hivyo, Msomi huyo aliyewahi kuwa mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) amefichua kwamba Serikali haitazingatia hoja, maoni na ushauri kutoka kwa Watanzania wakiwemo viongozi wa vyama vya siasa vya upinzani vinavyptolewa kwa kejeli na lugha alizodai siyo za staha dhidi ya viongozi wa CCM na Serikali.

Amewasihi Watanzania kuendeleza amani, tulivu, mshukamano na tabia ya kutofautiana kwa kujenga hoja kuwezesha Taifa kutumia rasilimali na fursa ya Kijiografia ya kuzungukwa na mataifa yasiyo na bandari kujinufaisha kiuchumi.

"Tanzania tumebarikiwa fursa ya Bahari na maziwa makuu ikiwemo Ziwa Victoria tunayomiliki takribani asilimia 51 yake, tutumie hiyo kama fursa kujiendeleza kiuchumi,’’ amesema Profesa Mkumbo ambaye kabla ya kuhamia CCM amewahi kuwa kada wa Chadema na ACT-Waalendo

Mwanasiasa mkongwe nchini, Stephen Wasira ameutuia mkutano huo kuihadharisha jamii dhidi ya matumizi mabaya ya maendeleo ya teknolojia, hasa mitandao ya kijamii akisema inaweza kupotosha ukweli ukitumika vibaya.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live
Related Articles: