Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Mbowe: Hatuna chuki na mkataba wa bandari

IMG 4340 Mbowe.jpeg Mbowe: Hatuna chuki na mkataba wa bandari.

Sun, 25 Jun 2023 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe amesema chama hicho hakina chuki wala hila katika msimamo wao wa kutokubaliana na hatua ya Serikali kuingia makubaliano na Serikali ya Dubai kuhusu uwekezaji wa bandari.

Oktoba 25, 2022, Serikali hizo mbili ziliingia makubaliano katika ushirikiano wa kiuchumi na kijamii kwa ajili ya uendelezaji na uboreshaji wa utendaji kazi wa bandari uendeshaji wa miundombinu ya kimkakati ya bandari za bahari na maziwa makuu, maeneo maalumu ya kiuchumi, maegesho ya utunzaji mizigo na maeneo ya kanda za kibiashara.

Mbowe ambaye ni mbunge wa zamani wa Hai mkoani Kilimanjaro ametoa msimamo huo jana Jumamosi Juni 24, 2023 wakati akizungumza na wanadaispora wa Uingereza, nchini humo. Katika mkutano huo Mbowe aligusuia masuala ya kijamii, kiuchumi na kisiasa.

“Hatupingi jambo kwa sababu tuna chuki, hila au wivu bali tunataka Taifa letu liwe mahali salama bora zaidi kwa kuishi. Chadema tulishauri kabla ya kupitishwa Serikali ya Tanzania na Zanzibar kuketi ili kuondoa sintofahamu na kasoro zilizopo, sambammba na kuwapa muda wananchi kuujadili,”amesema Mbowe.

Mbowe ambaye ni kiongozi wa zamani wa Kambi Rasmi ya Upinzani bungeni (KUB), amesema sakata hilo linagusa maslahi ya Watanzania wote bara na visiwani, akisisitiza suala hilo sio dogo na halitaishia katika mipaka ya Tanzania.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live
Related Articles: