Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Mahakama yampongeza wakili aliyefungua kesi sakata la Bandari

Wakili Mwambukusiiiii16).jpeg Mahakama yampongeza wakili aliyefungua kesi sakata la Bandari

Sat, 29 Jul 2023 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Mahakama Kuu Mbeya imempongeza Wakili Boniface Mwabukusi kwa weledi wake kisheria na kisiasa, katika kuiendesha kesi ya mkataba wa ushirikiano wa kiuchumi na kijamii, kati ya Serikali za Tanzania na Dubai (IGA), wenye lengo la kuwekeza na kuendesha bandari nchini.

Wakili Mwabukusi licha ya kufungua kesi hiyo mahakamani hapo kuwawakilisha wateja wake wanaoupinga mkataba huo, pia yeye binafsi amekuwa akiupinga vikali mkataba huo katika vyombo vya habari na mitandao ya kijamii na katika majukwaa ya kisiasa.

Katika kile kinachoonesha kuwa hata jopo la majaji walioisikiliza kesi hiyo limekuwa likimfuatilia katika majukwaa hayo, baada ya kuhitimisha usikilizwaji wa kesi hiyo jana Ijumaa, Julai 28, 2023, limetoa neno la kumpongeza kwa namna alivyokuwa anacheza vema kila eneo kwa wakati na staili yake.

"Kabla sijatamka tarehe ya uamuzi niseme mambo mawili matatu. Kwa niaba ya majaji wenzangu tunawashukuru sana mawakili kwa kile mlichokionesha. Mmeonesha the highest professionalism (weledi wa hali ya Juu) na wale walioko nyuma yenu wameona namna ambavyo mashauri haya yanaendeshwa," amesema Jaji Dunstan Ndunguru na kuongeza:

"Ninamshukru na kumpongeza sana Wakili Mwabukusi kwa namna alivyoweza kucheza sehemu zote mbili. Akiwa hapa mahakamani ameonesha professionalism kweli na nadhani hata wengine hamkuamini. Na akiwa kwenye uwanja wa siasa nako ameutumia vizuri na hivi ndivyo wengine pia wanavyopaswa kuwa."

Maneno hayo aliyoyasema Jaji Ndunguru ambaye ni Kiongozi wa jopo la majaji watatu waliosikilza kesi hiyo, kwa Wakili Mwabukusi yamefanya wasikilizaji wankesi hiyo waliokuwawamfurika ukumbini kulipuka kwa vicheko huku majaji wenyewe pia walishindwa kujizuia kucheka.

Majaji wengine katika kesi hiyo ni Mustafa Ismail na Abdi Kagomba.

Pia Jaji Ndunguru amewapongeza wananchi wote waliokuwa wanafuatilia kesi hiyo mahakamani hapo kwa kujitokeza kwa wingi kwenda kusikiliza kesi hiyo.

Baada ya kutamka hayo, Jaji Ndunguru amesema: “…niseme kwamba mahakama itatoa uamuzi wake Agosti 7, 2023 Jumatatu saa 3:00 asubuhi.”

Usikilizwaji wa kesi hiyo umehitimishwa leo na mawakili wa upande wa walalamikaji, ambao wamefunga pazia la usikilizwaji wa kesi hiyo kwa kuwasilisha hoja za ziada kujibu hoja za mawakili wa Serikali walizozitoa wakati walijibu hoja zao (mawakili wa walalamikaji)

Kesi hiyo ya Kikatiba namba 5 ya mwaka 2023 imefunguliwa na Watanzania wanne kutoka mikoa tofautofauti, Alphonce Lusako, Emmanuel Chengula, Raphael Ngonde na Frank Nyalusi dhidi ya Serikali.

Wadaiwa ni Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG), ambaye ni mshauri wa Serikali kwa mausuala ya kisheria, Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, Katibu Mkuu Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi na Katibu wa Bunge la Tanzania, ambaye ni mtendaji mkuu na mratibu wa shughuli za Bunge.

Katika kesi hiyo wanapinga makubaliano hayo yanayohusha uwekezaji katika Bandari za Tanzania zilizoko katika mwambao wa bahari na katika maziwa, kuwa ni batili kwa kuwa yana Ibara zinazokiuka Sheria na Katiba ya Nchi.

Pia wanadai kuwa mchakato wa kuridhia Bungeni ni batili kwa kuwa haukufuata utaratibu wa kisheria na bila kuwapa nafasi ya kutosha wananchi kutoa maoni yao kama sheria za nchi zinavyoelekeza.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live
Related Articles: