Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Bocco: Sijawahi kutangaza kustaafu soka

John Bocco JKT Tz Mshambuliaji mkongwe nchini, John Bocco

Tue, 3 Sep 2024 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Straika mkongwe nchini, John Bocco, ambaye kwa sasa ataitumikia JKT Tanzania, inayoshiriki Ligi Kuu Bara amesema hajawahi kutanganza anastaafu kucheza soka.

Kauli hiyo imekuja baada ya minong'ono ya muda mrefu ya mashabiki wa soka ambao walionyesha kushangazwa alipopewa 'thank you' na Simba, baadaye kuonekana akiifundisha timu ya vijana ya umri chini ya miaka 17, kabla ya  kutangazwa kusajiliwa na JKT Tanzania.

Kwa mara ya kwanza Bocco ameibuka juzi na kujibu kuwa alipokuwa akikifundisha kikosi cha vijana cha Simba, ilikuwa ni sehemu ya mafunzo yake ya ukocha kwa vitendo kwa sababu amekuwa akisoma huku akicheza soka na wala hakuwa amestaafu. Bocco pia alisema hata klabu yake ya zamani ya Simba haijawahi kutamka  nahodha wao amestaafu, badala yake wakamwaga kwa heshima zote.

Juzi ikicheza dhidi ya Azam FC, mchezaji hiyo aliichezea JKT Tanzania kwa mara ya kwanza, ikiwa ni timu yake mpya baada ya kuitumikia Simba kwa miaka sita. Bocco aliingia kipindi cha pili katika  mchezo huo uliochezwa kwenye Uwanja wa Meja Jenerali Isamuhyo, na timu hizo kutoka suluhu.

"Sijawahi kusema popote kama nastaafu mpira na wala Simba haijawahi kutamka mimi nastaafu kucheza soka. Kilichotokea waliniacha kwa heshima, na mimi nikaaga, nilikwenda kuifundisha timu ya Simba chini ya miaka 17 kama sehemu ya mafunzo kwa vitendo kwa kile ambacho nilikuwa nasomea," alisema Bocco.

Aliongeza aliamua kusomea ukocha mapema ili aje kuwa kocha mkubwa hapo baadaye kama ambavyo wanafanya baadhi ya wachezaji wakubwa Ulaya.

"Nimeanza kusoma mapema ili baadaye nije kuwa kocha mkubwa, niombeeni dua tu, na ndiyo malengo ya mtu yoyote anayetaka mafanikio, hata baadhi ya wachezaji Ulaya wanafanya hivyo, ila naona hapa nchini kimekuwa kitu cha ajabu kidogo," Bocco alisema.

Kuhusu kustaafu soka, alisema mpaka sasa hajafikiria hivyo, ila amebakisha misimu michache ili atundike daluga. "Sijajua mpaka sasa nina misimu mingapi mpaka nistaafu, lakini ni michache, siyo mingi, ila kwenye timu ya taifa tayari nimemaliza.

Hapa JKT Tanzania mimi ni mchezaji, wala siyo kocha mchezaji, au kocha msaidizi," aliongeza mchezaji hiyo ambaye amewahi kuitumikia Azam FC.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live
Related Articles: