Wachezaji wa Simba wanafahamu hesabu zilizopo kwao hivi sasa ni kuanza vizuri ugenini dhidi ya Al Ahli Tripoli ya Libya kisha kumaliza kazi nyumbani na kutinga makundi.
Jeuri kubwa waliyonayo Simba ni maboresho ya kikosi chao ambacho msimu huu kimeanza ligi kwa ushindi wa asilimia 100 kutokana na kukusanya pointi sita katika mechi mbili walizocheza wakifunga mabao saba huku nyavu zao zikiwa hazijatikiswa.
Miongoni mwa wachezaji wapya walioanza kwa moto mkali ni viungo Debora Fernandes Mavambo, Jean Charles Ahoua aliyehusika katika mabao matatu akifunga moja na asisti mbili, huku Awesu Awesu akiwa na bao moja. Pia Valentino Mashaka upande wa ushambuliaji amefunga mawili na kipa Moussa Camara ambaye ana clean sheet mbili katika ligi.
Keshokutwa Jumapili, Simba itakuwa kwenye Uwanja wa Tripoli, Libya kupambana na wenyeji wao Al Ahli Tripoli katika mchezo wa mkondo wa kwanza wa Kombe la Shirikisho Afrika.
Mchezo huo wa hatua ya kwanza, unatarajia kuanza saa 2:00 usiku kwa saa za Tanzania, kisha marudiano itakuwa Septemba 22 mwaka huu Uwanja wa Benjamin Mkapa, Dar es Salaam. Mshindi wa jumla wa mechi zote mbili atafuzu hatua ya makundi.
Simba ni miongoni mwa timu 12 zinazoanzia hatua ya kwanza moja kwa moja katika Kombe la Shirikisho Afrika msimu huu kutokana na idadi ya alama nyingi (39) ilizokusanya kwenye viwango vya CAF.
Beki wa kulia wa Simba, Shomari Kapombe amesema katika kipindi ambacho kila msimu huwa wanatamani sana kifike basi ni michuano ya kimataifa.
“Kinapofika kipindi cha mechi za kimataifa sisi wachezaji ndiyo tunakipenda zaidi na hata Wanasimba pia wanapenda, hivyo hatupo tayari kuona tunafanya makosa,” alisema Kapombe.
Kapombe aliyerejea Simba mwaka 2017 akitokea Azam, huu ni msimu wake wa nane akiwa ni beki tegemeo wa kulia kikosini hapo aliyechangia mafanikio katika michuano ya kimataifa na timu hiyo kuanzia 2018 hadi 2024 imecheza robo fainali tano, nne Ligi ya Mabingwa na moja Kombe la Shirikisho.
Beki huyo amesema ongezeko la wachezaji wapya msimu huu anaamini watafika mbali zaidi ya ilivyokuwa hapo awali.
“Naweza kusema hivi sasa matarajio ni makubwa kwa sababu kuna ongezeko la wachezaji wenye ari na nguvu ya kupambana na kujitolea kitu ambacho ni kizuri kama timu.
“Ni wakati sasa wa kufanya kwa vitendo kwa sababu maandalizi tuliyoyafanya na mbinu alizotupa mwalimu tunakwenda kuzionesha uwanjani.
“Kikubwa kila mchezaji yupo tayari kujitolea kuipambania timu kwa ajili ya kupata matokeo mazuri,” alisema Kapombe ambaye ana mkataba kikosini hapo hadi 2025.
Katika maboresho ya kikosi cha Simba msimu huu, uongozi wa timu hiyo umesajili wachezaji wapya 15 katika nafasi zote kuanzia kipa, beki, kiungo na ushambuliaji.
Wachezaji wapya msimu huu ni kipa Moussa Camara, mabeki Kelvin Kijili, Abdulrazack Hamza, Valentine Nouma na Chamou Karaboue. Viungo ni Jean Charles Ahoua, Awesu Awesu, Debora Fernandez Mavambo, Augustine Okejepha, Joshua Mutale, Omary Omary na Yusuf Kagoma. Kwa upande wa washambuliaji wapo Valentino Mashaka, Steven Mukwala na Leonel Ateba.