Wakati Simba ikiwa njiani kwenda Libya kuvaana na Al Ahli Tripoli, kocha wa Wekundu hao, Fadlu Davids amefunguka jinsi alivyopangwa kuwasapraizi wenyeji wao katika mechi hiyo ya mkondo wa kwanza ya raundi ya pili ya Kombe la Shirikisho Afrika kwa mbinu atakazowapa mastaa wa kikosi hicho.
Simba iliyoapangwa kuanzia raundi hiyo ya pili itakuwa wageni wa Al Ahli Jumapili, jijini Tripoli kabla ya kurudiana nao wiki moja baadae jijini Dar es Salaam na mshindi wa jumla atatinga makundi, ili kuanza msako wa taji hilo linaloshikiliwa kwa sasa na Zamalek ya Misri iliyowafunga RS Berkane ya Morocco.
Mwanaspoti iliwahi kuitaarifu kuwa, wapinzani wa Simba wamejinoa vilivyo, huku ikitoa mkataba wa mwaka mmoja kwa kocha wa kikosi hicho Chokri Khatoui, kwa sharti la kuivusha timu hiyo katika mchezo huo dhidi ya Simba, baada ya awali kuing’oa Uhamiaji ya Zanzibar katika raundi ya kwanza kwa ushindi wa jumla wa mabao 5-1 mechi zote zikipigwa Libya.
Simba imekuwa ikishiriki michuano ya Ligi ya Mabingwa tangu 2018/19 japo mwaka juzi ilitolewa na kuangukia Shirikisho ilipoishia robo fainali na msimu huu imerejea tena Shirikisho baada ya kumaliza nafasi ya tatu katika Ligi Kuu Bara na kupangwa kuanzia raundi hiyo ya pili.
Akizungumza na Mwanaspoti kabla ya kuondoka nchini, Kocha Fadlu alisema mchezo huo na timu ya Libya hautakuwa rahisi kwa kuwa wanakwenda kukutana na kikosi kinachotaka mabadiliko ya mafanikio katika soka la Afrika na tayari amejiandaa kuwashangaza wakiwa ugenini.
Alisema anafahamu mechi itakuwa na presha hasa kwa dakika 25 za kwanza kwa kila kipindi ambapo wameshajipanga sawa sawa.
“Hatuendi kuzuia ila kucheza soka la kushambulia ili wapate ushindi, ambao utawapunguzia presha katika mechi ya marudiano. Mechi kama hizi hazina nafasi nyingi lakini kitu muhimu kwa wachezaji wangu ni kuzitumia nafasi za kutosha kadiri watakavyo zitengeneza,” alisema Fadlu na kuongeza;
“Hata kama tunakwenda kutafuta ushindi tutahakikisha tunakuwa na nidhamu kwenye kujilinda ili wapinzani wetu wasipate nafasi ya kutufunga, lakini kutakuwa na mabadiliko makubwa katika kikosi kitakachocheza huko,” alisema Fadlu.
Alfajiri ya jana kikosi cha Simba kilisepa kwenda Libya na kikiwa na jumla ya wachezaji 22 na kilitakiwa kwanza kifike Uturuki kabla ya kutimkia kwa Walibya kwa ajili ya mechi hiyo itakayopigwa Jumapili kuanzia saa 2:00 usiku.
Wachezaji waliotajwa katika msafara huo ni makipa Ally Salim, Aishi Manula na Mousa Camara, huku mabeki wakiwa ni Shomari Kapombe, Kelvin Kijili, Mohammed Hussein, Valentin Nouma, Che Fondo Malone, Karaboue Chamou na Abdurazak Hamza, huku viungo ni; Augustine Okejepha, Debora Mavambo, Awesu Awesu, Yusuf Kagoma, Joshua Mutale, Edwin Balua, Fabrice Ngoma, Jean Ahoua na Kibu Denis, huku washambuliaji ni Steven Mukwala, Valentino Mashaka na Lionel Ateba
Balua, Mukwala, Mohammed Hussein, Ally Salim na Camara walikuwa vikosi vya timu za taifa na wataungana na wenzao huko huko Libya.