Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

AG awashangaa wanaosema mkataba wa bandari ni miaka 100

Mwanasheria Mkuu Wa Serikali (AG), Jaji Eliezer Feleshi Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Jaji Dkt. Eliezer Feleshi

Mon, 26 Jun 2023 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Jaji Dkt. Eliezer Feleshi, amejitosa kwenye mjadala wa uwekezaji wa kampuni ya Dubai ya DP World unaotarajiwa kufanywa kwenye bandari ya Dar es Salaam kwa kusema kuwa kuna upotoshaji mkubwa usio na tija katika mjadala huo.

Akizungumza kwa mara ya kwanza katika mahojiano maalumu ofisini kwake Dodoma, Jaji Feleshi amesema kuwa upotoshaji huo unaweza kuifanya Tanzania ionekane kama inabagua wawekezaji kutoka nchi fulani.

"Mtu anasema mkataba ni wa miaka 100 na hiyo ilikuja hata kabla Bunge halijaazimia. Wengine wanasema ni mkataba wa maisha. Unatafuta hicho kipengele cha maisha unapekua kifungu kimoja mpaka mwisho, hakuna," alisema Feleshi.

Ameonya pia kuwa lugha za kibaguzi zinazotolewa na baadhi ya watu dhidi ya wawekezaji kutoka nchi fulani zinaweza kuharibu sifa ya Tanzania kama taifa linaloongoza kuvutia watalii kwenye ukanda huu wa Afrika.

"Je sasa tunataka tujenge mazingira ya kuwatia hofu wawekezaji kwamba nchi yetu haitaki wawekezaji?" Alihoji Jaji Feleshi.

Aliongeza kuwa Tanzania imekuwa inajulikana kama nchi ambayo haifungamani na upande wowote miaka mingi na inayokaribisha wawekezaji kutoka sehemu zote duniani.

"Leo unapoanza kuona Waarabu ni kama shida, unachagua (wawekezaji watoke) wapi?" Aliongeza.

Mwanasheria Mkuu wa Serikali pia amepangua upotoshaji kuwa bandari ya Dar es Salaam inauzwa kwa kusema kuwa hakuna kipengele chochote kwenye mkataba kati ya Tanzania na Dubai (intergovernmental agreement au IGA) kinachozungumzia uuzwaji wa Bandari.

"Tunaposema bandari imeuzwa, je ni kweli imeuzwa? Kile kiambatisho kimeeleza maeneo ya mahusiano kwa mujibu wa ile ibara ya 4 ni kwenye gati ngapi kati ya ngapi na hizo zinazobaki ni ngapi," alisisitiza.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live
Related Articles: