Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Watatu Prisons kuikosa Simba

Watatu Prisons Watatu Prisons kuikosa Simba

Mon, 2 Oct 2023 Chanzo: Mwanaspoti

Wachezaji watatu, kipa Benedict Tinoco, Ibrahim Abraham na Nurdin Chona huenda wakaukosa mchezo ujao wa Ligi Kuu dhidi ya Simba kufuatia majeraha waliyonayo.

Hata hivyo pamoja na kutajwa kwenye orodha hiyo, kipa Tinoco tangu atue kikosini humo katika dirisha dogo msimu uliopita hajawahi kudaka mechi yoyote, huku Yona Amos, Edward Mwakyusa wakionekana kulishawishi benchi la ufundi na Mussa Mbisa ambaye naye hajacheza kutokana na majeraha aliyokuwa nayo.

Prisons inajiandaa na mchezo wake wa Ligi Kuu dhidi ya Wekundu hao Oktoba 5 ambapo hadi sasa haijaonja ushindi wowote kwenye mechi tatu ilizocheza na kuwa mkiani kwa pointi moja.

Maafande hao pia wanawakabili wapinzani hao na wawakilishi wa nchi kwenye michuano ya klabu bingwa Africa sawa na watani zao yanga wakikumbuka kupoteza mechi zote walipokutana msimu uliopita ikiwamo kisago kizito cha 7-1 jijini Dar es Salaam.

Mchezo baina ya timu hizo unatarajia kupigwa Alhamisi, Octoba 5 mwaka huu kwenye uwanja wa Sokoine jijini hapa ukiwa wa kwanza kwa Prisons kucheza nyumbani baada ya mechi tatu kuwa ugenini walipoambulia pointi moja, huku wakipoteza miwili na kuruhusu mabao sita, wakifunga mawili tu.

Akizungumza wakati wa mazoezi ya leo, Afisa habari wa timu hiyo, Jackson Mwafulango amesema wachezaji hao wanasumbuliwa na majeraha hivyo mechi ijayo huenda wakakosekana.

"Tinoco ameanza mazoezi ila siyo kwa ubora, lakini Chona na Abraham nao waliumia kwenye mechi dhidi ya Azam wakisumbuliwa na goti," amesema Mwafulango.

Mwafulango amesema pamoja na kuwakosa nyota hao, benchi la ufundi chini ya kocha mkuu, Fred Felix 'Minziro' ataamua kuwapanga nani kutokana aina ya mchezo kwani kikosi Prisons inacho kikosi bora na imara.

Katika hatua nyingine, Afisa habari huyo ameelezea kuanzishwa kwa timu ya Wanawake ambayo itashiriki Ligi ya Mkoa kuanzia msimu huu akibainisha kuwa kuanzia wiki hii itaanza mazoezi, huku usajili ukiendelea.

"Ni rasmi Prisons Queens imeanza na mazoezi yake yatakuwa yakifanyika Jumatatu, Jumatano na Ijumaa, japokuwa kikosi hakijatimia na uongozi unawakaribisha wachezaji wenye uwezo waje kujaribu bahati, tumejipanga kimkakati na hii ndio Prisons" amesema Mwafulango.

Chanzo: Mwanaspoti
Related Articles: