Kijamii

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Lifestyle

SIL

MenuKijamiiMaoni
Articles

Vita ya Tripoli bado mbichi Temeke, Deborah ajipange

Simba Wajipangeeeeeeeeeeeeee.jpeg Vita ya Tripoli bado mbichi Temeke, Deborah ajipange

Wed, 18 Sep 2024 Chanzo: Mwanaspoti

Haikuwa sehemu salama Tripoli. Simba waliwasili Tripoli miaka 13 tangu kuuawa kwa Rais wa zamani wa Libya, mwenye nchi yake. Muammar Muhammad Abu Minyar Al Gaddafi. Bado haikuwa sehemu salama kwa Simba ndani na nje ya uwanja.

Nje ya uwanja unaweza kujua kwanini Walibya waliwahi kufungiwa wasicheze na mashabiki. Wana shangwe ambalo limeambatana na vurugu. Walidhihirisha kwa wachezaji wa Simba. Walifanikiwa kufanya vurugu ikiwemo kuwarushia chupa wachezaji wa Simba.

Ndani ya uwanja waliwaonyesha Simba kwamba wana timu. Ni kweli wana timu. Vita iliwayumbisha hapa katikati kiasi cha kufungwa na Biashara United ya Shinyanga. Lakini na hapo hapo Simba walitumia nafasi hiyo kuwaonyesha Al Ahly Tripoli kwamba wao ni nani. Sawa, na Simba pia wamepitia katika wakati mgumu miezi 36 iliyopita. Walipata anguko.

Ni anguko ambalo lilisababisha wajikute katika michuano hii baada ya kushika nafasi ya tatu msimu uliopita. Na katika msimu huu ambao wanajaribu kuibuka ndipo wamejikuta katika michuano hii. Simba haikuwa timu ya kwenda Tripoli kucheza michuano ya Shirikisho, lakini wamekwenda. Na bahati nzuri walikwenda na timu ambayo inafufuka.

Na walionyesha kwamba wanafufuka. Kwanza kwa namna ambavyo walicheza kwa ari na kitimu. Kocha Fadlu Davis ameonyesha anatengeneza timu ambayo inashindindana. Sina hofu sana kwamba miezi 15 iliyopita Simba wangeweza kupoteza pambano Tripoli. Namna ambavyo wenyewe walikuwa wanaonana ingewapoteza Simba mapema.

Lakini, Simba hii mpya inacheza kitimu na mchezaji mmoja mmoja kuna ongezeko kubwa. Kitimu ni namna ambavyo waliweza kuwazuia wenyeji wasipate bao kwa dakika tisini mbele ya mshambuliaji wao hatari, Agostinho Mabululu. Walijipanga wengi mbele ya mpira na kwa ushirikiano uliotukuka.

Na hapo hapo tunazungumzia mtu mmoja mmoja. Inaanzia kwa kipa wa Simba, Moussa Camara. Ametulia. Mtu wa kwanza ambaye hapaswi kutetemeka katika mazingira kama haya ni kipa. Anaweza kufungwa kwa kutetemeka tu. Mara ya mwisho Simba kufanya vizuri katika mazingira ya chuki kipa alikuwa nyota wao wa mchezo, Juma Kaseja, mwaka 2003 wakati Simba walipowatoa Zamalek ugenini.

Camara hakutetemeka, lakini zaidi tuna kijana wetu, Hamza Abdulrazak. Beki wa mpira. Mtulivu kama alivyo. Anacheza mpira wa miaka ya mbele yake. Simba imejipiga chenga ya mwili na Hamza ameokoa jahazi. Simba walimsajili beki, Chamou Karaboue kutoka Asec Mimosas wakiamini angetengeneza pacha nzuri na Che Malone. Hata hivyo Hamza ameingia kati.

Kwa macho yangu Chamou ni mzito. Ana umbo kubwa, lakini kwa mechi za kwanza ambazo nimemuangalia sijaona kama anaweza kufikia ule uwezo wa kina Josh Onyango na Serge Wawa katika ubora wao. Kabla mambo hayajaharibika mbeleni Hamza amejitokeza kuokoa jahazi. Hakusajiliwa kwa mbwembwe sana lakini ghafla ameibuka kuwa tumaini.

Hamza ana kimo kizuri. Ana utulivu, ana akili ya mpira, ana nguvu, ana kila kitu. Moyo wangu unapata liwazo ninapojikumbusha kwamba safu ya ulinzi itaendelea kuwa salama kwa muda mrefu ujao. Tuna kina Dickson Job, Bakari Mwamunyeto, Ibrahim Bacca. Tuna Hamza pia. Kuna wakati aliwahi kuitwa katika kikosi cha timu ya taifa. Hatujui kwanini hakuendelea kuitwa. Hata hivyo muda mchache ujao anaweza kuitwa.

Kuna Yusuf Kagoma. Bonge la mchezaji. Wakati Simba walipokuwa wanampigania Lameck Lawi kati yao na Coastal Union nilisafiri na Kagoma na Lawi kwenda Indonesia katika mechi ya kirafiki kati ya Taifa Stars dhidi ya Indonesia. Niliona sababu zote za Simba kumuwania Kagoma na siyo Lawi. Kagoma ni mtu na nusu.

Lawi alionekana kutetemeka katika mechi ya kawaida ambayo haikuwa na presha kubwa. Kagoma alicheza kama vile nilivyokuwa namuona Singida Fountain Gate. Anajua mpira halafu msela. Ana ‘kiburi’.

Napenda wachezaji vizuri. Kiburi chanya. Mpira huwa hauwashindi. Kinachowashinda ni pale kiburi cha nje ya uwanja kinapozidi.

Kagoma ni mchezaji wa aina hii. Wale wachezaji ambao achilia mbali kujua mpira, lakini wanacheza huku mioyo yao ikiwa na inaongea ikisema “nyie wote wajinga mimi najua mpira”. Kuna faida ya kuwa na kiburi chanya. Katika uwanja uliosheheni chuki kama ule wa juzi ulimhitaji sana mchezaji kama yeye ndiyo maana Kagoma hakuyumba.

Akili yangu iko palepale. Taifa Stars. Hawa ndio wachezaji wakusutusaidia mbele ya safari. Kwanini inakuwa bora zaidi wakicheza timu hizi kubwa kama Simba na Yanga? Kwa sababu wanacheza mechi nyingi za kimataifa katika klabu zao.

Inatusaidia. Kina Shomari Kapombe, Jonas Mkude, Mohammed Hussein ‘Tshabalala’, John Bocco walitusaidia sana pale Stars kwa kucheza Simba iliyokuwa inafika mbali.

Kagoma pia anaibeba Simba kuficha lolote lililo na upungufu katika usajili wa Augustine Okajepha. Ukiwachunguza kwa karibu unagundua kwamba Kagoma yupo mbele hatua kadhaa. Rafiki yetu kutoka Nigeria bado anajitafuta.

Mpira wetu haueleweki. Siyo kila anayekuja kwa matarajio huwa anayafikia kwa haraka. Na tukienda kwa wageni tuna Joshua Mutale. Rafiki yetu kutoka Zambia. Mutale labda ndiyo maana aliendelea kubaki Zambia licha ya kutajwa hapa na pale kwamba ni mchezaji mzuri.

Anacheza bila malengo. Anakimbia bila malengo. Mbio zipo, kasi ipo, dhamira yake ipo. Tatizo ni akili yake ya mwisho. Analingana na baadhi ya wachezaji wetu. Halafu tuna Deborah Fernandes Mavambo.

Fundi wa mpira. Ana kila kitu ambacho kiungo anapaswa kuwa nacho. Jicho la mbali, nguvu, umiliki wa mpira, mnyumbuliko na kila kitu. Mtu na nusu. Kama kuna mchezaji anaipa sana Simba nguvu katika sehemu ya kiungo ni Deborah. Ataimiliki Simba kwa muda mrefu kadri atakavyojisikia.

Tatizo kubwa la Simba lipo eneo la mbele. Bado sijawaelewa vizuri kina Leonel Ateba na Steven Mukwala. Maeneo mengi hasa ya kiungo cha chini na nyuma wanaonekana wapo salama. Tatizo lipo eneo la mbele.

Wanahitaji kuimarika zaidi. Pambano lile pale Tripoli hawakupiga hata shuti moja ambalo lililenga lango. Na sasa kuna kesi kubwa ya kujibu pale Temeke wikiendi ijayo.

Mechi bado haijafa. Wageni watakuwa bado wana timu imara kama ilivyokuwa wiki iliyopita ambapo waliliweka lango la Camara majaribuni. Na tusubiri kuona kitakachotokea. Halitakuwa pambano rahisi sana.

Columnist: Mwanaspoti
Related Articles: