Katika hali isiyo ya kawaida, wapinzani wa Simba, Al Ahli Tripoli wamekodi walinzi binafsi ‘bodyguards’ kwa ajili ya kuwalinda wachezaji pamoja na benchi la ufundi pindi kikosi kitakapotua Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere, Dar es Salaam.
Al Ahli Tripoli inatarajiwa kuwasili Dar es Salaam saa tatu asubuhi ya leo kwa ajili ya kucheza mchezo wa marudiano kutafuta tiketi ya kufuzu hatua ya makundi Kombe la Shirikisho Afrika dhidi ya Simba.
Mchezo huo utachezwa Jumapili ya wiki hii Septemba 22, 2024 kwenye Uwanja wa Mkapa, Dar es Salaam baada ya ule wa awali nchini Libya kumalizika kwa matokeo ya 0-0.
Mmoja kati ya watu waliokuja kuwapokea ambaye hakutaka jina lake kuandikwa, ameliambia Mwanaspoti kuwa wameandaa ulinzi huo kwani wanahofia kufanyiwa fujo.
“Jamaa wanaogopa kutokana na yaliyotokea kule kwao, hata hapa tulipo hatujaambiwa wanafikia hoteli gani, hadi wafike ndio tutajua,” alisema mtu huyo.
Ikumbukwe kwamba, baada ya mchezo wa wikiendi iliyopita uliochezwa nchini Libya na timu hizo kushindwa kufungana, iliripotiwa mashabiki wa Al Ahli Tripoli waliwafanyia fujo wachezaji wa Simba wakati wanarudi vyumbani. Pia ilielezwa wachezaji wa timu hiyo na viongozi waliwashambulia waamuzi.
Mbali na hilo, kipa wa Simba, Aishi Manula iliripotiwa alipigwa na ofisa mmoja aliyekuwa akiimarisha usalama uwanjani.