Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Waarabu kumng'oa Robertinho Simba

Robertinho Hgs.jpeg Waarabu kumng'oa Robertinho Simba

Tue, 2 May 2023 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Simba imerejea juzi ikitoka Morocco ilipotolewa kiume kwenye Ligi ya Mabingwa Afrika, lakini kama kuna kitu kimezusha gumzo kwa wekundu hao ni ubora wao uwanjani na sasa kama kuna mtu anayesakwa ni kocha wao Robert Olivieira 'Robertinho'.

Mezani kwa Robertinho linakuthibitishia kuna ofa mbili kubwa ambazo inategemea na akili kubwa ya mabosi wa Simba na uamuzi wa kocha huyo raia wa Brazil.

Tuanze na Misri klabu ya Al Ittihad, inayoshiriki ligi kuu nchini humo imempigia simu kocha huyo ikitaka huduma yake baada ya kuona hesabu zao za kuingia ndani ya klabu tatu za juu kuwa na mashaka.

Al Ittihad sasa inafundishwa na kocha wa zamani wa Simba, Zolan Maki ambaye kabla ya kutua huko alitokea hapa nchini wakiona bado hawajakubali mwendo wa kocha wao huyo raia wa Serbia.

Katika mechi zao tano za mwisho Al Ittihad imeshinda mechi moja na kupoteza tatu huku wakitoa sare moja hatua ambayo imewatisha mabosi wa klabu hiyo wakianza mchakato wa siri.

Mbali na Al Ittihad ofa nyingine kubwa ni ile kutoka Angola ambako Robertinho aliwahi kufanya kazi miaka ya nyuma ambako nako wamemwekea mzigo mrefu.

Klabu ya Atlético Sport Aviação ambayo amewahi kuifundisha Mbrazil huyo kwa miaka miwili na kuiacha katika nafasi nzuri inapiga hesabu pia na kumrudisha kocha huyo katika nafasi yake hiyo huku kufuru ikiwa ni fedha za malipo yake.

Akizungumzia jana kwa kifupi Robertinho licha ya kukiri ofa kuwa nyingi kwake alisema kwa sasa anataka kukutana na mabosi wa Simba kuhakikisha wanamaliza msimu vizuri kwa mashindano ya ndani.

"Ofa hizi ni nyingi kila siku, ni kweli hizo taarifa ninazo lakini kwa sasa nipo hapa Simba, tumetoka safari leo (jana), kitu ambacho kipo kichwani kwangu sasa ni kumaliza kwanza huu msimu kwa kuhakikisha tunafanya vuzuri kulingana na malengo yetu, baadaye tukimaliza msimu nitaongea na viongozi wa klabu," alisema Robertinho.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live
Related Articles: