Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

TV

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Upepo mbaya, matukio 9 yaliyotikisa michezoni Oktoba

Oktoba Pic Data Matukio yaliyotikisa Oktoba

Sun, 31 Oct 2021 Chanzo: www.mwanaspoti.co.tz

Zilikuwa siku 31 ngumu kwenye familia ya michezo nchini kwa mwezi Oktoba unaoelekea ukingoni ambao umetikisa sekta hiyo.

Ukiachana na kipigo ilichokipata Simba Oktoba 24 kilichowatoa machozi baadhi ya mashabiki wa timu hiyo, Oktoba umekuwa ni mwezi mgumu kwa wanamichezo wengi nchini kwenye anga za kimataifa.

Haya ni matukio tisa makubwa yaliyotikisa familia ya michezo katika mwezi Oktoba.

BIASHARA UNITED

Licha ya ushindi wa mabao 2-0 ilioupata nyumbani, timu hiyo ilikwama kusafiri kwenda nchini Libya kwenye mchezo wa marudiano wa raundi ya pili wa Kombe la Shirikisho barani Afrika dhidi ya wenyeji, Al Ahli Tripoli, uliokuwa uchezwe Oktoba 23 kwenye mji wa Benghazi.

Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) liliwasiliana na Shirikisho la Soka Afrika (Caf) kuomba mchezo huo usogezwe hadi Oktoba 27 kutokana na changamoto ya usafiri wa anga lakini hadi tunakwenda mitamboni Biashara United wanaendelea kusubiri majibu.

AZAM NJE KIMATAIFA

Oktoba 23, upepo mbaya uliendelea kwa matajiri wa Chamazi, Azam FC kutupwa nje ya michuano ya Kombe la Shirikisho Afrika.

Timu hiyo iliruhusu kipigo cha bao 1-0 dhidi ya wenyeji, Pyramids lililofungwa na Ally Gabri Mossad katika dakika ya 29 kwenye uwanja wa Jeshi la Anga wa Juni 30 jijini Cairo, Misri.

Kipigo hicho kiliifanya Azam kutupwa nje kwenye mashindano ya kimataifa baada ya suluhu katika mchezo wa kwanza kwenye Uwanja wa Azam Complex.

SIMBA SC YASHTUA

Jumapili ya Oktoba 24, ilikuwa siku ngumu kwa wapenzi na mashabiki wa Simba nchini ambao hawakutarajia matokeo ya kikatili ambayo timu yao ilikumbana nayo kwenye Uwanja wa Mkapa, Dar es Salaam kutoka kwa Jwaneng Galaxy ya Botswana.

Simba ambayo mechi ya kwanza ilishinda ugenini jijini Gaborone, Botswana kwa mabao 2-0, ilijikuta ikichapwa nyumbani kwa mabao 3-1 na kuondoshwa kwenye Ligi ya Mabingwa Afrika kwa jumla ya mabao 3-3 huku Jwaneng Galaxy ikisonga mbele kwa kanuni ya mabao ya ugenini.

Awali, Simba iliichapa Galaxy mabao 2-0 , lakini ikatolewa kwa kuruhusu mabao zaidi nyumbani Oktoba 24 na kutupwa nje kwenye michuano hiyo lakini ikaangukia kwenye Kombe la Shirikisho Afrika ambako imepangiwa Red Arrows ya Zambia.

TWIGA STARS CHALI

Upepo mbaya uliendelea Oktoba 23 kwa timu ya taifa ya soka ya wanawake, Twiga Stars kuondoshwa katika mbio za kuwania tiketi ya kucheza Fainali za Mataifa ya Afrika (Afcon).

Twiga ilipokea kipigo cha mabao 3-2 kutoka kwa Namibia kwenye Uwanja wa Dobsonville jijini Johannesburg, Afrika Kusini na kuondoshwa kwa jumla ya mabao 5-3 baada ya kufungwa nyumbani mabao 2-1 mchezo wa kwanza.

GOMES ATIMULIWA

Oktoba 26 itabaki kwenye historia ya klabu ya Simba baada ya kufikia hatua ya kuachana na kocha mkuu, Didier Gomes Da Rosa ikiwa ni siku mbili baada ya timu hiyo kuondoshwa kwenye Ligi ya Mabingwa Afrika.

Pia, klabu hiyo iliwapa mkono wa kwaheri kocha wa makipa, Mbrazili Milton Nienov na kocha wa viungo, Mtunisia Adel Zrane.

Hata hivyo, licha ya mashabiki kukubaliana na uamuzi wa kumtimua Gomes, lakini waliwapa presha viongozi wakitaka Zrane arejeshwe kwani hawaoni kosa lake.

DULLAH MBABE ATIKISA

Baada ya kipigo cha Oktoba 9, bondia Abdallah Pazi ‘Dullah Mbabe’ alielezea kupumzika kupanda ulingoni, huku kipigo hicho dhidi ya Mkongomani Tshimanga Katompa kikigeuka gumzo nchini.

Mbabe, bondia namba mbili nchini kwenye uzani wa super middle alichapwa vibaya nyumbani na Katompa - pambano lililowasikitisha mashabiki wengi.

ETTIENE AFUNGUA DIMBA

Oktoba 24 iliacha doa kwa Kocha Ettiene Ndayiragije ambaye amekuwa wa kwanza wa Ligi Kuu kutimuliwa msimu huu.

Klabu ya Geita Gold ambayo inashiriki Ligi Kuu Bara kwa mara ya kwanza ilitangaza kumtupia virago kocha huyo Mrundi baada ya kuiongoza timu hiyo katika mechi nne za ligi na akipoteza mbili ugenini na sare mbili nyumbani.

Kabla ya kutua Geita Gold, Ndayiragije aliwahi kuzifundisha timu za Mbao FC ya Mwanza, KMC na Azam FC za Dar es Salaam na timu ya Taifa ya Tanzania ‘Taifa Stars’ kwa nyakati tofauti, ambako pia aliacha rekodi fulani zilizombeba mpaka akatua Geita.

MTANGO AIKOSA ABU

Matokeo ya sare yaliyotolewa na majaji Oktoba 13 yalimuweka kando na ubingwa wa Afrika, bondia Salum Mtango aliyekuwa akizipiga nyumbani jijini Dar es Salaam.

Mtango, bondia namba moja nchini kwenye uzani wa super light alishindwa kutamba mbele ya Hannock Phiri wa Malawi baada ya majaji wote kutoa matokeo ya sare kwa mabondia hao.

NDONDI ZA DUNIA

Mabondia wa timu ya taifa, Yusuph Changarawe, Alex Sulwa na Kassim Mbundwike waliondolewa kwenye mchezo kwa kutotokea ulingoni (walkover) kwenye mashindano ya dunia ya ngumi za ridhaa yanayoendelea nchini Serbia. Timu hiyo ilipaswa kucheza Oktoba 26, 27 na 28.

Chanzo: www.mwanaspoti.co.tz
Related Articles: