Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Chadema wazuiwa kuwatembelea waathirika wa mafuriko ya Hanang

Lema Mboweee.jpeg Chadema wazuiwa kuwatembelea waathirika wa mafuriko ya Hanang

Thu, 7 Dec 2023 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Ujumbe wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), unaoongozwa na mwenyikiti wake Taifa, Freeman Mbowe, umedai kuzuiwa na Jeshi la Polisi kutembelea wahanga wa maporomoko ya udongo katika mji mdogo wa Katesh, wilayani Hanang, Mkoa wa Manyara.

Taarifa hizo zimesambaa leo Alhamisi, katika mitandao ya kijamii, ambapo mmoja kati ya ujumbe huo ambaye ni mjumbe wa Kamati Kuu ya Chadema, Godbless Lema, ameandika katika ukurasa wake wa mtandao wa X, kuwa wamelazimika kukatisha safari yao kutokana na changamoto hiyo.

“Tumekatisha safari ya kuelekea Katesh - Hanang kuona wahanga wa mafuriko kutokana na vikwazo vingi tulivyokutana navyo, kuanzia tunaingia Manyara na zaidi vikwazo vikali tulipotaka kusalimia wagonjwa Hospitali ya Rufaa Mkoa wa Manyara. Tunaendelea kuwapa pole sana wakazi wote Manyara. Tutaongea na vyombo vya habari kwa taarifa ya kina zaidi,” ameandika Lema.

"Kada mwingine wa Chadema, Boniface Jacob, kupitia mtandao huo aliandika akidai tangu asubuhi, Mbowe na wenzake, wamezuiwa na Jeshi la Polisi mkoani Manyara, kutembelea eneo lolote lililokumbwa na maafa.

“Viongozi wa CHADEMA waliomba kwenda maeneo tofauti ambayo hayapo katika ratiba ya kutembelewa na Rais Samia, lakini pia Jeshi la polisi limekataa wasiende popote wala kuonana na majeruhi yoyote wilayani Hanang, pamoja na kukataliwa kupokelewa misaada yake kwa wahanga,” ameandika Jacob na kuongeza:

“Mwenyekiti alikuwa amebeba misaada mbalimbali ya  dawa za binadamu pamoja na vifaa vingine kwa ajili ya kuwagawia waathirika wa mafuriko hayo”

MwanaHALISI imemtafuta Kamanda wa Jeshi la Polisi mkoani manyara, George Katabazi kupitia njia ya simu, ili kupata ukweli juu ya madai hayo, ambapo namba zake zilikuwa hazipatikani.

Tayari Rais Dk. Samia Suluhu Hassan, amewasili Katesh kwa ajili ya kuwapa pole wahanga wa janga hilo lililotokana na maporomoko ya sehemu ya miamba dhoofu ya Mlima Hanang, ambayo yalishindwa kuhimili mgandamizo kutokana na kunyonya maji.

Kaya zaidi ya 1,000 zimeripotiwa kuathirika na janga hilo lililosababisha vifo 69 na kujeruhi watu takribani 100.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live
Related Articles: