Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Umeiona Simba mpya ya Benchikha?

Azam Simba Sz Umeiona Simba mpya ya Benchikha?

Wed, 14 Feb 2024 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Licha ya kuwa bado Kocha wa Simba, Abdelhak Benchikha ana kazi kubwa ya kuendelea kukisuka kikosi chake kutokana na maboresho yaliyofanywa dirisha lililopita la usajili, angalau kwa sasa mashabiki wa Wekundu hao wa Msimbazi wanapumua kutokana na mwenendo wa timu yao.

Awali mashabiki wa Simba walipoteza imani na timu yao hasa baada ya kukumbana na mvua ya mabao 5-1 kutoka kwa watani zao wa jadi, Yanga kwenye Dabi ya Kariakoo, jambo lililowafanya mabosi wa timu hiyo, mosi kumfuta kazi aliyekuwa kocha wa timu hiyo, Roberto Oliveira ‘Robertinho’ kisha vikaanza vikao vya hapa na pale.

Yote hayo yalifanyika kwa ajili ya kutafuta ufumbuzi ambao pengine unaweza kuwarejesha kwenye makali yao, pamoja na kelele za mashabiki ndipo mabosi wa timu hiyo walipoafikiana na kumpa jukumu hilo, kiboko wa Yanga, Benchikha aliyeiongoza USM Alger kutwaa ubingwa wa Kombe la Shirikisho Afrika msimu uliopita.

Tangu Mualgeria huyo kukabidhiwa kijiti cha Robertinho, Novemba 28 mwaka jana, 2023 hadi leo (Jumatano), ametimiza siku 78 ni miezi mitatu kasoro, tayari dalili njema zimeanza kuonekana kwenye kikosi hicho kilichopoteza matumaini ya Wanasimba ambao baadhi yao walishaanza kuwanyooshea vidole viongozi.

Benchikha ambaye bado hajapoteza mchezo wowote kwenye ligi, ameiongoza Simba kwenye jumla ya michezo 16 ya mashindano yote, ikiwemo sita za Kombe la Mapinduzi na Wekundu wa Msimbazi walipoteza kwenye fainali kwa kufungwa bao 1-0 na Mlandege.

Takwimu zinaonyesha Benchikha ameshinda mechi 10 ambazo nne ni kwenye Kombe la Mapinduzi dhidi ya JKU (3-1), Singida FG (2-0) katika hatua ya makundi huku wakiendeleza ubabe kwenye robo kwa kuifunga Jamhuri bao 1-0 kisha wakaifunga tena Singida kwenye nusu kwa mikwaju ya penalti 3-2 baada ya kutoka sare ya bao 1-1.

Mechi nyingine ambazo ameingoza Simba kuibuka na ushindi ni kwenye ligi dhidi ya Kagera Sugar (3-0) na huo ndio ulikuwa ushindi wake wa kwanza tangu ajiunge na vigogo hao kisha akalipa kisasi kwa Wydad Casablanca kwa kuwatandika mabao 2-0 kwenye Uwanja wa Mkapa.

Katika mechi nne za mwisho kwa Simba kwenye ligi, imeshinda tatu huku zote zikiwa ugenini, dhidi ya Mashujaa (1-0), Tabora United (4-0) na Geita Gold (1-0), pia waliitandika Tembo FC kwenye Kombe la FA ‘ASFC’ kwa mabao 4-0 kabla ya mechi hizo.

Benchikha amepoteza mechi mbili tu, ya kwanza ya Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya Wydad Casablanca kwa bao 1-0, nyingine ilikuwa fainali ya Kombe la Mapinduzi visiwani Zanzibar.

Kocha huyo anayependelea kutumia mfumo wa 4-2-3-1, ametoka sare kwenye mechi nne, moja ya Ligi ya Mabingwa na ndio ilikuwa mechi yake ya kwanza kuiongoza Simba ilikuwa Botswana dhidi ya Jwaneng Galaxy (0-0), nyingine ilikuwa kwenye Kombe la Mpinduzi dhidi ya APR (0-0).

Upande wa Ligi, ilikuwa dhidi ya KMC kwa mabao 2-2 kwenye uwanja mgumu ambao mashabiki wa Simba wamekuwa wakiamini kwa upande wao kupata matokeo ‘Azam Complex’ na mechi nyingine ilikuwa dhidi ya Azam FC (1-1).

Simba chini ya Benchikha imepachika jumla ya mabao 26 katika mashindano yote hivyo ina wastani wa kufunga bao 1.6 kwenye kila mchezo huku ikiruhusu mabao sita tu (wastani 0.3) kwenye michezo 16.   MAINGIZO MAPYA    Benchikha aliyezaliwa Novemba 22, 1963 (60) alikifanyia tathimini kikosi chake na akapima majukumu ambayo waajiri wake walimpa, aliamua kupitisha fagio dirisha dogo hasa eneo la ushambuliaji kwa ajili ya kuongeza makali katika safu hiyo.

Katika mazingira ambayo hakuna aliyetegemea, Simba iliachana na washambuliaji wake wawili, mmoja akitolewa kwa mkopo, Moses Phiri na Jean Baleke, wakaingia Freddy Michael Kouablan raia wa Ivory Coast kutoka Green Eagles ya Zambia na Mgambia, Pa Omar Jobe.

Kocha huyo pia aliona kuna haja kuwa na kiungo mwingine wa kati kwa ajili ya kuimarisha eneo hilo licha ya kuwa na Mzamiru Yassin, Sadio Kanoute na Fabrice Ngoma ndipo akasajiliwa Babacar Sarr.

Nyota hao pamoja na wengine ambao walisajiliwa dirisha dogo tayari wameanza kuingia kwenye mfumo wa kocha huyo na wapo ambao wameanza kuonyesha makeke yao mfano mzuri ni Sarr ambaye aliifanya Simba kuibuka na ushindi kwenye mchezo wao wa mwisho kwenye ligi dhidi ya Geita akikamilisha idadi ya wageni hao kufunga kwenye mechi za ligi tangu wametua.

USAJILI KIMKAKATI Benchikha mjanja kweli, wachezaji wa kigeni ambao amesajili wote wanaongea vizuri Kifaransa kwani mbali na lugha mama ya nchini kwao ya Kiarabu kocha huyo ana uwezo mzuri wa kuongea lugha hiyo.

Ukiitazama Simba zaidi ya asilimia 80, nyota wake wa kigeni wanaongea lugha hiyo hivyo ni rahisi kwake kufanya nao mawasiliano katika kuwasilisha mpango wake wa kimbinu, hata hivyo wazawa nao wamekuwa na nafasi ya kucheza kwenye kikosi chake mfano mzuri ni Shomary Kapombe, Mohammed Hussein na hata Kibu Denis.

YEYOTE FRESHI Miongoni mwa vitu ambavyo Benchikha amekuwa akivifanya ni pamoja na kutoa nafasi kwa kila mchezaji ambaye huonekana kuwa tayari kimchezo kama kushindwa ushindwe mwenyewe kuonyesha makali yako.

Wachezaji ambao wameonekana kutumika zaidi kwenye kikosi hicho tangu kutua kwake Msimbazi ni Tshabalala bado Simba haijapata mchezaji wa kutoa changamoto kwa beki huyo wa kushoto, mwingine ni Che Malone kutokana na kutokuwepo kwa Henock Inonga Baka ambaye alikuwa Ivory Coast kwa fainali za Mataifa ya Afrika.

Malone ndiye beki kiongozi aliyesalia kwenye eneo la kati hivyo ilibidi kutumika sambamba na Kennedy Juma au Hussein Kazi, maeneo mengi mara kwa mara kocha huyo alionekana kufanya mabadiliko kulingana na mpango alionao kwenye mchezo husika na amekuwa akipata matokeo mazuri.

MWENYEWE AFUNGUKA Wakati akitambulishwa kuwa kocha mpya wa Simba, Benchikha aliwahidi Wanasimba kuwapa raha hivyo anaeleza yupo kwenye mchakato wa kuendelea kukijenga kikosi hicho huku akihakikisha wanaendelea kufanya vizuri.

“Shauku yangu ni kuona timu ikiendelea kufanya vizuri, ligi ni ngumu na tuna mashindano mengine mbele yetu hivyo tunatakiwa kuwa bora na tayari kukabiliana na yeyote,” alisema kocha huyo.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live
Related Articles: