Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Sven apiga simu Simba, Mo Dewji atua Dar

Sven.jpeg Sven apiga simu Simba, Mo Dewji atua Dar

Tue, 14 Nov 2023 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Simba chini ya kaimu kocha mkuu, Daniel Cadena imerejea mazoezini na mambo matatu, lakini Mwanaspoti linajua Mbelgiji Sven Ludwig Vandenbroeck amepiga simu kwa tajiri akiomba apewe kazi.

Habari za uhakika zinasema Sven aliyeachana na Simba kiroho safi 2021 na kumuachia mikoba ya muda Matola ameomba kazi.

Habari zinasema kocha huyo amewaambia Simba kuwa yupo tayari kupokea kijiti pale alipoachia na anaamini uzoefu alioupata nchi za Kiarabu utatosha kuivusha.

Hata hivyo, uongozi unatarajiwa kufanya uamuzi wa nani kocha mkuu kuanzia leo kwani mwezeshaji, Mohammed Dewji ‘MO’ tayari amerejea nchini juzi.

Kwa mujibu wa habari muda wowote kuanzia leo wanamaliza mchakato kwani kocha watakayempitisha anapaswa kuwepo nchini kuishuhudia mechi ya Asec.

Pamoja na Sven, Mwanaspoti linajua Simba wamezungumza na Nasreddine Nabi ambaye ni kocha wa zamani wa Yanga pamoja na Abdelhak Benchikha wa USM Algers. Sambamba na hao kuna maombi kibao yametumwa ingawa hakuna kocha mzawa.

Vanderbroeck aliiongoza Simba kwenye mechi 69 za mashindano, zikiwemo za kirafiki na kushinda 53, sare 10 na kufungwa sita.

Katika kipindi hicho aliiwezesha kutwaa mataji matatu ya Ngao ya Jamii, Ligi Kuu Bara na Kombe la Shirikisho la Azam (ASFC).

Na alisepa siku moja baada ya kuiwezesha Simba kufuzu hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika baada ya ushindi wa mabao 4-0 dhidi ya FC Platinum ya Zimbabwe,jijini Dar es Salaam.

MIKAKATI YA CADENA

Cadena, kocha wa makipa akisaidiana na nguli, Seleman Matola ambao wanakaimu baada ya Roberto Oliveira ‘Robertinho’ kupigwa chini wameanza kufumua na kuisuka upya timu hiyo kwenye Uwanja wa Mo Simba Arena bila Henock Inonga, Clatous Chama, Kibu Denis, Mzamiru Yassin, Said Ntibazonkiza na Aishi Manula walio katika timu za taifa.

Simba inahesabu siku 12 kabla ya kucheza na Asec Mimosas ya Ivory Coast mchezo wa kwanza wa hatua ya makundi wa Ligi ya Mabingwa utakaopigwa Novemba 24 kwenye Uwanja wa Mkapa.

Ili kuhakikisha inashinda mechi hiyo na kuanza kibabe hatua hiyo, Cadena na Matola wameuomba uongozi kuwatafutia mechi za kirafiki tatu zenye ushindani ambazo zitawapa tathmini nzuri.

Cadena aliliambia Mwanaspoti, kazi kubwa ya kwanza kwao ni kuwajenga wachezaji kisaikolojia kukubali matokeo yaliyotokea na kuanza upya kutengeneza kikosi imara. “Simba ina wachezaji wengi bora. Tunachofanya sasa ni kuwataka wajiamini kwanza na wakubali kubadilika, kisha kwa pamoja tutengeneze timu itakayocheza vizuri na kutupa matokeo chanya,” alisema.

“Tutacheza mechi tatu hadi nne za kirafiki ambazo zitatupa picha mpya ya kikosi na wapi pa kuanzia katika mechi zijazo,” alisema Cadena huku beki wa zamani wa Simba, Boniphace Pawasa akishauri timu hiyo kujifungia ili kutengeneza kikosi na kuachana na kelele za upotoshaji.

“Kinachotakiwa ni kuangalia kilicho mbele yao. Wajipange kwa ajili ya mechi zijazo mambo ya nje ya uwanja wawaachie watu wa nje, lakini benchi la ufundi na wachezaji watimize majukumu na hapo watafanya vizuri bila shida,” alisema Pawasa.

Mchezaji na kocha wa zamani wa timu hiyo, Jamhuri Kihwelo ‘Julio’ alisema: “Hakuna timu isiyofungwa duniani kote. Simba imepoteza mechi moja tu na msimu bado unaruhusu kuinuka na kufanya mapinduzi. Wasikate tamaa bali wafanye kila kitu kwa usahihi na wanaweza kushangaza mwishoni mwa msimu.”

TUZO YA MASHABIKI

Mashabiki wa Simba juzi usiku walitwaa Tuzo ya Mashabiki Bora wa michuano mipya ya African Football League (AFL).

Mechi mbili tu dhidi ya Al Ahly, zilitosha kuiaminisha Afrika kuwa mashabiki wa Simba ni bora zaidi kuliko wa nchi za Kiarabu.

Waliwashinda wale wa Al Alhy, Petro de Luanda, Esparence, TP Mazembe, Wydad AC, Enyimba na mabingwa wa michuano hiyo kwa mara ya kwanza, Mamelodi Sundowns.

Mamelodi ilitwaa ubingwa huo kwa kuichapa Wydad AC kwa mabao 2-0 katika fainali ya pili iliyopigwa juzi Afrika Kusini baada ya ile ya kwanza iliyochezwa Morocco kupoteza kwa mabao 2-1, hivyo kutwaa taji kwa jumla ya mabao 3-2.

DHIDI YA ASEC

Kabla ya mechi ya Novemba 24 ya Simba, mastaa wa zamani na makocha wameishauri kitu.

Nyota wa zamani wa Yanga na Taifa Stars, Mohamed Hussein ‘Mmachinga’ alisema inahitaji kuweka sawa mambo matatu akiyataja kuwa ni utulivu, umoja na mshikamano na kusahau yaliyopita.

“Simba kinachowatesa ni kitu kidogo tu, mchezo dhidi ya Yanga kufungwa bao nyingi vile. Sasa wanatakiwa kuungana kuondoa makundi ndani ya timu na kuwa kitu kimoja, naamini wataweza kupambana na wanaanzia nyumbani. Kuhusu kikosi wanacho kizuri tu sema wawe na utulivu,” alisema Mmachinga.

Mchezaji wa zamani wa Simba, Fikiri Magoso alisema: “Simba ya Roberthino ilikuwa na matatizo makubwa, inafunga lakini inafungwa mabao ya ajabu na laini sana. Kwa wasiojua mpira walikuwa wanawalaumu mabeki lakini ukweli fomula ya huyo kocha haikueleweka.”

Aliongeza kuwa hata utimamu wa miili ya wachezaji wanapaswa kuwa nao zaidi ya ule wa sasa, huku kocha wa Kagera Sugar, Mecky Maxime akisema kitakachoigharimu ni kuweka kichwani yaliyopita.

“Naona Simba ina wachezaji wazuri sema watulize vichwa na kuiangalia mechi kwa ukubwa wake,” alisema.

Philpo Alando, nyota wa zamani wa Azam FC alisema, “Hakuna nafasi hata ya kumpata mchezaji mwingine hadi dirisha dogo ambalo nalo ni muda mfupi na hata mashabiki wanatakiwa kujua timu yoyote duniani inapitia wakati mgumu hivyo wanatakiwa kuwapa moyo.”

Chanzo: www.tanzaniaweb.live
Related Articles: