Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Sunzu awapa ujumbe mabeki Simba

Inonga X Che Malone Mzuka Sunzu awapa ujumbe mabeki Simba

Wed, 18 Oct 2023 Chanzo: Mwanaspoti

Wakati saa zikiendelea kusogea kuelekea mchezo wa michuano mipya ya African Football League (AFL) kati ya Simba na Al Ahly ya Misri, safu ya ulinzi ya Wekundu wa Msimbazi imepewa nondo muhimu za kuzingatia kuhakikisha haifanyi makosa yatakayowagharimu kwenye mtanange huo utakaopigwa Ijumaa.

Mchezo huo utakaonogeshwa na sherehe za ufunguzi rasmi wa michuano hiyo utakaofanyika katika Uwanja wa Benjamin Mkapa, jijini Dar es Salaam kisha kurudiana Oktoba 24, mwaka huu jijini Cairo, Misri ambapo mshindi wa matokeo ya jumla atatinga nusu fainali.

Ujumbe huo umetolewa leo Jumatano Oktoba 18, 2023 na straika wa zamani wa Simba, Felix Sunzu, aliyesisitiza ameitazama timu hiyo katika baadhi ya mechi za Ligi Kuu Bara na kubaini mabeki wa pembeni na makipa wamekuwa wakifanya makosa ambayo kama watapata mpinzani hatari basi wataadhibiwa.

Sunzu aliyejiunga na Simba mwaka 2011, akitokea Al Hilal ya Sudan, ameliambia Mwanaspoti kwa njia ya simu kwamba safu ya ulinzi ya Simba, inapaswa kuongeza umakini katika ukabaji wa mtu mmoja kwa mmoja, kutia presha wanapopoteza mpira huku akishauri kipa atakayeanza kwenye mchezo huo awe anazungumza na mabeki kuwakumbusha wajibu na kuanzisha mipira kwa umakini.

“Niliwatazama mchezo dhidi ya Singida Big Stars kulikuwa na tatizo la full backs (mabeki wa pembeni), hawakuwa makini sana kwa sababu kama Singida wangekuwa na washambuliaji hatari, basi Simba wangepoteza huo mchezo, sasa makosa kama haya huwezi kuyafanya kwa Waarabu hasa pembeni mwa uwanja, umakini uongezeke, wakiweka presha na wewe unaweka tusiwaachie kwani ukiwa makini na wao wanachoka,” amesema Sunzu na kuongeza;

“Wale ni wajanja ukiwaachia tu ukasinzia wanakufunga hiyo haitakiwi, kosa lolote kwenye ulinzi na kipa. Sijajua kipa gani ataanza kwa sababu nina wasiwasi na Manula (Aishi) hawezi kutoka kwenye majeraha ukaanza mchezo mkubwa hivyo lakini ni kipa mzuri anayeweza kuisaidia timu kwenye mchezo kama huu, kipa atakayepangwa atulize mabeki, aongee awe mzuri kwenye kuanzisha mipira, kwa hiyo hata huyo Salim (Ally) ni kipa mzuri anaweza tu kucheza.”

Mshambuliaji huyo raia wa Zambia, amesema benchi la ufundi la Simba linapaswa kupiga hesabu zake vizuri katika uchaguzi wa mastraika wa kuanza katika mtanange huo, ambapo amependekeza aaminiwe Mkongomani, Jean Baleke na Moses Phiri badala ya John Bocco ambaye amekuwa akipewa nafasi kubwa siku za karibuni.

“Tatizo la sasa la Simba ni kule mbele hawana mshambuliaji hatari kariba ya Fiston Mayele ambaye anaweza kumiliki mpira, kufunga mabao na kumaliza mechi, Bocco (John) amekuwa akipata nafasi kubwa ya kucheza lakini kiukweli siyo mtu wa kumuanzisha katika mechi hii labda wamuangalie Baleke (Jean) wamuanzishe asipokupa unachotaka kipindi cha pili aingie Phiri (Moses),” amesema Sunzu aliyetwaa taji la Ligi Kuu na Simba msimu wa mwaka 2011/2012.

Chanzo: Mwanaspoti
Related Articles: