Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Siri ya mashujaa wa kibegi cha Simba

Shujaaa Siri ya mashujaa wa kibegi cha Simba

Mon, 7 Aug 2023 Chanzo: Mwanaspoti

Wakati Tamasha la ‘Simba Day’ likihitimishwa jana Jumapili moja ya jambo kubwa lililogonga vichwa vya habari hapa nchini ni kibegi cha timu hiyo ambacho kilitumika kwa ajili ya uzinduzi wa jezi katika mlima mrefu Afrika, Kilimanjaro.

Kibegi hicho kilichojizoelea umaarufu na kuteka hisia za wengi kutokana na promosheni kubwa iliyopigwa kuanzia kimetangazwa hadi Ijumaa ya Julai 21, mwaka huu zilipozinduliwa jezi za msimu huu saa 1:00 usiku.

Wakati kibegi hicho kikizungumzwa sana wapo wahusika ambao walitumika kukifikisha kwenye mlima huo huku usiri mkubwa baina yao kwa wao ukiwa chachu ya kutokuvujisha hadi pale malengo yao yalipotimia.

Mwanaspoti limezungumza na mwanachama wa timu hiyo, Julius Kiwale mwenye kadi namba 5215 na kuelezea safari ilivyokuwa.

NAFASI ALIIPATAJE?

Kiwale anasema wakati viongozi wa timu hiyo wanatangaza mchakato huo alimpigia simu, Ofisa Mtendaji Mkuu wa Simba, Imani Kajula na kumuelezea nia yake ya kutaka kupata nafasi ya kuwepo miongoni mwa watu wa kuandika historia.

“Sio mara ya kwanza kupanda Mlima Kilimanjaro japo nilipanda zaidi ya miaka 10 iliyopita, baada ya kumweleza aliniamini na kuniambia kutokana na utayari wangu, basi ananiteua nami nikatengeneze historia na timu yangu.”

UVUMILIVU

Anasema unapotaka kupanda mlima huo ni lazima uwe na mvumilivu mkubwa kutokana na mazingira magumu yaliyopo ya hewa ndio maana wengi wao licha ya kutamani kufika ila hujikuta wakiishia njiani na kushindwa kuendelea.

“Unapoanza safari kuna muda unakosa hamu ya kula kutokana na baridi kali jambo linalosababisha wengi wao kushindwa kumudu, ni suala la kuomba tu Mungu kwa sababu licha ya mimi kupanda awali ila ilikuwa pia shida.”

HUPIMWA AFYA

Anasema kabla ya kupanda mlima huo ni lazima kwanza upeleke cheti chako ulichopimwa afya ili iwe rahisi kwa madaktari kutambua unakabiliwa na changamoto gani ili utakapopata shida waangalie namna ya kukutibu.

“Unywaji wa pombe au pilipili ni vitu ambavyo havitakiwi kwa sababu vinapunguza ile hali ya unywaji wa maji kwa wingi, kwani unapokuwa kwenye mlima wataalumu wanashauri sana unywe lita nne za maji kwa siku husika,” anasema Kiwale wakati alipokuwa wakifanya mazungumzo haya na Mwanaspoti.

UAMINIFU

Anasema haikuwa rahisi kuficha siri iliyopo kwenye kibegi hadi walipofika na kutimiza malengo yao licha ya kukutana na ushawishi kutoka kwa watu mbalimbali waliokuwa wanataka wakifungue na kuona kilichokuwa ndani.

“Katika ile safari mimi peke yangu ndiye nilikuwa mkubwa, hivyo niliwaambia vijana wenzangu kuaminiwa kwetu ni mtaji sana, hivyo tutunze siri kwa manufaa ya maisha yetu baadaye na kiukweli tuliweza na kufanikiwa mno.”

CHANGAMOTO

Katika kila jambo lenye mafanikio basi changamoto nazo hazikosekani kwani Kiwale anasema mojawapo ni muda hafifu.

“Wataalamu wanashauri kupanda juu ya mlima kuanzia saa 5 usiku ili ikupe morali ya kuamini ni karibu kwa sababu huoni mbele ila sisi kutokana na muda mchache ilibidi tupande asubuhi kitu ambacho kilikuwa shida.

“Sababu ya kupanda asubuhi ni ili tuwahi kupiga picha ambazo zitatumika kutambulisha jezi siku ile ya usiku, pia kitaalamu unatakiwa kuupanda kwa siku tano hadi wiki ila sisi tulipanda kwa siku tatu kutokana na muda.”

BEI YA KUPANDA MLIMA

Anasema bei za kupanda mlima huo zinatofautiana ila kima cha kawaida ni Sh1.6 milioni ambapo kupitia fedha hizo utapatiwa wataalumu utakaoongozana nao wakiwemo mpishi wa chakula, atakayekubebea vifaa na daktari.

UMAARUFU KUONGEZEKA

Kiwale anasema moja ya jambo kubwa alilofaidika nalo katika safari hiyo ni kupata marafiki wengi ambao hapo awali hawakuwa wakijuana huku akiweka wazi umaarufu wake pia umeongezeka kwa kasi tofauti na ilivyokuwa.

“Wazazi wangu walinishangaa sana waliposikia nimepanda mlima kwa sababu niliapa sitapanda tena ila baada tu ya Simba kunipa nafasi nikaona niitumie vyema na nashukuru japokuwa nisingependa kuweka wazi fedha nilizopata.”

USHAURI

Anasema mwitikio ni mdogo sana kwa Watanzania kupanda mlima wetu jambo ambalo hata Wazungu wanaotutembelea kutoka mataifa mbalimbali wanatushangaa, hivyo anaomba tuwe na kipaumbele zaidi kuutangaza utalii wa nchi yetu.

“Shida kubwa kwetu sisi (Watanzania) ni uoga ila tusifikie huko kwa sababu kuna bibi wa miaka 86 na mzee mwenye miaka 76 ambao walipanda na kushuka sasa nashangaa kwa vijana wenzangu wanajiweka nyuma sana na fursa zilizopo nchini kwetu.”

MASHUJAA WENGINE

Mbali na Kiwale ila mashujaa wengine waliopanda mlima huo na kibegi ni Michael Mushi, Sebastian Marco, David Tarimo, Calvin Swai na Joseph Alex ambao watatambulishwa kwenye tamasha la Simba Day leo Jumapili kama sehemu ya kuwapa heshima kwa kitendo walichokifanya.

Chanzo: Mwanaspoti
Related Articles: