Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Singida yahusishwa na Kocha mwingine wa Simba SC

Pablo X Gomes Singida yahusishwa na Kocha mwingine wa Simba SC

Fri, 6 Oct 2023 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Singida Big Stars jana ilikuwa uwanjani Turiani, Morogoro kuvaana na Mtibwa Sugar katika mechi ya Ligi Kuu Bara, huku mabosi wa klabu hiyo wakianza rasmi kusaka kocha mpya atakayekinoa kikosi hicho na makocha Pablo Franco na Didier Gomes waliowahi kuinoa Simba kwa vipindi tofauti wakitajwa.

Singida inayonolewa na kaimu kocha mkuu, Ramadhan Nswanzurimo kwa sasa imekuwa haina kocha mkuu baada ya Mjerumani, Ernst Middendorp kutimka Septemba 19, mwaka huu ikiwa ni muda mchache tangu ajiunge na timu hiyo.

Taarifa kutoka ndani ya timu hiyo ililiambia Mwanaspoti, mazungumzo baina ya viongozi wa Singida na makocha hao yanaendelea na kama mambo yataenda sawa basi mmoja kati yao atapewa mikoba ya kukiongoza kikosi hicho.

“Ni kweli tumekuwa kwenye mazungumzo na makocha mbalimbali lakini bado hatujafikia makubaliano yoyote, sisi kama viongozi hatutafanya maamuzi ya haraka kwa sababu ya kile kilichotokea mwanzo,” kilisema chanzo chetu.

Kwa upande wa Makamu wa Rais wa klabu hiyo, Ibrahim Mirambo akizungumzia juu ya makocha hao, alisema hata yeye amekuwa akisikia tu kuhusu taarifa hizo ila wao kama viongozi bado wana imani na benchi lilolopo sasa.

“Sijajua hizo taarifa zinatoka wapi ila ninachojua mimi tuna benchi bora la ufundi ambalo linaweza kuongoza timu hadi pale tutakapoamua vinginevyo, nisingependa kuzungumzia sana kuhusu tetesi za mitandaoni,” alisema.

Mwanaspoti linatambua, Nswanzurimo ambaye ni Mkurugenzi wa Ufundi viongozi wangetamani kuendelea kuifundisha hadi mwisho wa msimu ingawa itategemea na kiwango ambacho timu hiyo itaonyesha katika michezo mbalimbali.

Timu hiyo ilianza msimu na Mholanzi, Hans Van de Pluijm aliyeiwezesha kufuzu michuano ya Kombe la Shirikisho Afrika huku akiiongoza katika mchezo mmoja tu wa Ligi Kuu Bara na Tanzania Prisons ulioisha 0-0, Agosti 22, mwaka huu.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live
Related Articles: