Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Simba yawapiga 'stop' Akpan, Okwa kucheza Ihefu

Okwaaa Akpan Akpan na Okwa wakiwa Ihefu

Thu, 6 Apr 2023 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Wakati Simba ikitarajiwa kucheza mechi yake ya robo fainali ya Kombe la Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) dhidi ya Ihefu kesho, klabu hiyo imewapiga 'stop' nyota wake, Nelson Okwa na Victor Akpan ambao wapo kwa mkopo kucheza dhidi yao.

Meneja Habari na Mawasiliano wa klabu ya Simba, Ahmed Ally alisema jana kuwa Okwa na Akpan hawatocheza kesho kwenye mechi hiyo kwa sababu ya makubaliano ya mkataba wa mkopo ambayo waliwapa Ihefu.

Alisema siyo kwenye mechi hiyo tu, bali hata mechi ya Ligi Kuu Tanzania Bara itakayochezwa Aprili 10 kwenye Uwanja wa Highland Estates, Ubaruku, Mbarali, Mbeya.

"Akpan na Okwa ni wachezaji wetu ambao wapo Ihefu kwa mkopo na kwenye makubaliano yetu ni kwamba hawatocheza kwenye mechi yoyote dhidi yetu," alisema Ahmed.

Okwa na Akpan ambao wote ni raia wa Nigeria walipelekwa kwa mkopo kipindi cha dirisha dogo la usajili katika klabu hiyo baada ya kuonekana hawana nafasi kwenye kikosi cha kwanza cha Simba.

"Kuna mikataba ya aina mbili, ya kumruhusu mchezaji kucheza kwenye timu aliyotoka na upo ambao hamruhusu kuichezea timu ya mkopo dhidi ya timu mama.

"Na zipo sababu za kitaalam hapo ambazo zinasababisha vitu vyote hivyo ikiwemo upangaji wa matokeo, timu inayommiliki mchezaji ambaye wanamlipa, inaweza kutumia mwanya huo huo kumshawishi, yaani acheze chini ya kiwango kwenye mechi ya timu yake ya mkopo dhidi ya timu yake mama,” alisema Ally.

Aliongeza: “Na siyo hivyo kuna mengi tu yaliyo kinyume chake na yanayofanana na hayo, kwa hiyo kuepusha hivyo ndiyo ikaja hiyo mikataba na ipo duniani kote, kwa maana hiyo sisi kwa Akpan na Okwa hawatocheza kwenye mechi zote ambazo Ihefu watacheza dhidi yetu."

Simba ambayo ilianza mazoezi Jumanne iliyopita mara baada ya kurejea kutoka nchini Morocco ilikokwenda kucheza mechi ya kukamilisha ratiba ya Ligi la Mabingwa Afrika Kundi C dhidi ya Raja Casablanca, itarudiana na Ihefu kwenye Uwanja wa Uhuru, Dar es Salaam na mshindi wa mechi hiyo atacheza na Azam FC ambayo imetinga hatua ya nusu fainali baada ya kuifunga Mtibwa Sugar mabao 2-0.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live
Related Articles: